• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kamati yapinga LSK kutaka bunge livunjwe

Kamati yapinga LSK kutaka bunge livunjwe

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC), imepuuzilia mbali shinikizo za Chama cha Wanasheria Nchini za kutaka bunge livunjwe kwa kushindwa kupitisha sheria ya kufanikisha usawa wa jinsia bungeni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Muturi Kigano, jana alisema kuvunjwa kwa bunge wakati huu hakutamfaidi raia wa kawaida ambaye anakabiliwa na changamoto za kiuchumi na janga la Covid-19.

“Kuvunjwa kwa bunge wakati huu hakutakuwa na faida yoyote kwa raia wa kawaida, ambao tayari wameathirika na makali ya corona ambayo yamesababisha matatizo mengi ya kiuchumi. Sheria na Katiba inapasa kutekelezwa kwa njia inayomsaidia mwananchi sio kumuumiza,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo jana.

Bw Muturi, ambaye ni Mbunge wa Kangema, alisema suala hilo la usawa wa kijinsia katika mabunge yote mawili limeshughulikiwa kwa undani kwenye ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Nahimiza LSK isubiri mapendekezo ya ripoti hiyo kuhusu suala hilo yatolewe kwa umma. Baada ya hapo JLAC itachambua mapendekezo hayo na kuwasilisha ripoti kamili kwa bunge lote,” akasema.

“Hitaji kubwa la Wakenya wakati huu sio kushiriki uchaguzi, kwani watapata nafasi ya kushiriki zoezi hili miaka miwili kuanzia sasa. Taifa halifai kutekwa nyara na sheria,” Bw Kigano akaongeza.

Mnamo Alhamisi wiki jana, Rais wa LSK Nelson Havi aliwasilisha ombi kwa Jaji Mkuu David Maraga akimtaka kumshauri avunje bunge kwa kutopitisha sheria hiyo ya kufanikisha hitaji kwamba angalau thuluthi moja ya wabunge na maseneta ni wanawake.

Maombi mengine ya aina hiyo yaliwasilishwa kwa Bw Maraga na aliyekuwa Mbunge wa Marakwet Magharibi David Sudi, Margaret Toili, Fredrick Mbugua, Bernhard Aoko na mwanaharakati Stephen Owoko.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka, ambao pia walipokea nakala za maombi hayo, wamepewa muda wa wiki kusema ni lini mabunge hayo yatapitisha sheria hiyo.

Wakifeli kufanya hivyo, Bw Maraga atakuwa huru kumshauri Rais Kenyatta avunje bunge, hatua ambayo itapelekea wabunge 349 na maseneta 67 kupoteza nafasi zao.

Kwa mujibu wa kipengele cha 27 (8) cha Katiba angalau thuluthi moja ya wanaoshikilia nyadhifa za kuchaguliwa na kuteuliwa wanafaa kuwa wa jinsia tofauti.Lakini wakati huu, kwa mfano, kuna jumla ya wabunge 72 wa kike kati ya 349 ilhali Katiba inahitaji idadi wabunge hao kuwa angalau wabunge 117.

Bunge la kitaifa limejaribu mara nne kupitisha sheria ya kufanikisha hitaji hilo la kikatiba lakini likafeli.

Jaribio la mwisho, la Novemba 2019, lilifeli baada ya idadi tosha ya wabunge (angalau 233) kukosa kufikiwa kuwezesha mswada wa sheria hiyo upigiwe kura.

You can share this post!

Gideon aweka mikakati kuteka nyoyo za vijana

Maseneta wakosa kuelewana kwa mara ya saba

adminleo