Walioshukiwa kumuua kondakta kwa kuongeza nauli waponea
Na RICHARD MUNGUTI
MAAFISA wawili wa chama cha matatu cha Mwiki waliofikishwa kortini kwa mauaji ya kondakta aliyeongeza nauli kwa Sh20 tu waliachiliwa huru Alhamisi baada ya ripoti ya upasuaji kubaini alifariki kutokana na ugonjwa wa kichomi au Pneumonia.
Washukiwa hao Mabw John Kibe Nyagah na Geoffrey Ngamau Wambui walidaiwa walihusika na mauaji ya Julius Kamau Mburu.
Hakimu mkazi Bi Miriam Migure aliwaachilia huru baada ya kukabidhiwa ripoti ya afisa wa upasuaji.
“Sababu ya kufariki kwa Mburu ilikuwa ni kichomi na wala sio majeraha alyokuwa nayo,” alisema Bi Mugure akiongeza “Polisi wataendelea na uchunguzi na iwapo watapata ushahidi ambao unawaweza kuwafungulia mashtaka basi watatiwa nguvuni na kushtakiwa.”
Wawili hao walitiwa nguvuni baada ya polisi kusema hawatekelezi kazi yao ilhali marehemu alifichua kabla ya kuaga alikuwa ameshambuliwa na wao.
Akiwasilisha ombi la kutaka wazuiliwe kuchunguzwa na kuhojiwa kiongozi wa mashtaka Bi Agatha Lango alisema utingo huyo alikumbana na mauti kwa madai ya kuwaongezea abiria nauli kwa Sh20 tu.
Magari ya matatu siku hiyo ya Aprili 23, 2018 yalikuwa yanalipisha Sh80 lakini marehemu anadaiwa aliongeza nauli ikafika Sh100.
Bi Lango aliomba mahakama iwazuilie Mabw Nyagah na Ngamau kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo.
Pia alisema cheti cha upasuaji wa maiti kubaibinisha kilichosababisha kifo cha Mburu kinahitajika kuambatanishwa katika nakala za ushahidi.
Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ilisema Mburu aliuawa Aprili 23, 2018.
Upande mashtaka uliomba wawili hao wazuiliwe kwa siku saba lakini wakili Daniel Ndegwa akapinga akisema siku moja au mbili zatosha kuwezesha polisi kukamilisha shughuli za upasuaji.
“Polisi hawahitaji siku saba kufanyia maiti upasuaji,” alisema Bw Ndegwa .
Bw Ndegwa alisema katiba yakataza mmoja kuzuiliwa kwa kipindi kirefu korokoroni pasi kuelezwa mashtaka watakayofunguliwa.
Mahakama ilifahamishwa kuwa washukiwa hao wawili walijisalamisha kwa kituo cha Polisi cha Central kuhojiwa baada ya kupashwa habari kuwa walikuwa wanasakwa.
Hakimu mkazi Bi Mirriam Mugure aliamuru washukiwa hao wawili wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Central kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi.
Washtakiwa watafikishwa kortini kujibu shtaka la kumuua Mburu.