Habari Mseto

Wasiwasi barakoa zilizotumika zikiendelea kutupwa ovyo

August 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Serikali imeeleza wasiwasi wake kuhusu utupaji kiholela maski zilizotumika ikisema utepetevu huo unatia watu katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona iwapo waliozivalia walikuwa wameugua.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman amesema kiwango ambacho maski zinaonekana kutupwa katika maeneo ya umma kama vile masoko, vituo vya matatu, kandokando mwa barabara na njia na pia katika vituo vya garimoshi vinazua hofu.

“Tunapaswa kujitahadhari tunavyotupa maski ili kuepuka uchafu wa mazingira na kuhatarisha maisha yetu wenyewe,” Waziri akaonya.

Pia, alihimiza wahudumu wa afya kuwa kielelezo kwa umma katika suala la maski na vifaa vya kuzuia kuambukizwa (PPE) corona baada ya kuvitumia.

Dkt Aman alisema utafiti wa wataalamu wa afya umeonyesha chembechembe za virusi vya corona (Covid-19) vinasalia kwenye maski kwa walioambukizwa.

Alisema utupaji wa maski kiholela unawaweka katika hatari watoto, na ambao ni vigumu kuwadhibiti wanapocheza.

Aidha, Waziri alionya kuwa maski zilizotumika na kutapakaa zinapofurushwa na upepo ni hatari kwa watu.

“Tuwajibike tunapotoa maski na kutupa zilizotumika mahali zinakofaa, na kwa mujibu wa maelekezo ya Idara ya Afya. Kimsingi, utupaji wa taka kiholela ni hatari na ni kuchafua mazingira. Taifa hili lina takriban watu milioni 50, hebu jiulize sote tukitupa maski kiholela hali itakuwaje?” Waziri akahoji, akidokeza kwamba Wizara ya Afya inashirikiana kwa karibu na serikali za kaunti kuibuka na mikakati maalum ya utupaji maski.

Alisema usafi wa mazingira wakati huu taifa linaendelea kuhangaishwa na janga la Covid-19 unapaswa kuwa wa hadhi ya juu.

Waziri pia alisema Wizara ya Afya kwa ushirikiano na serikali za kaunti zinaendelea kuimarisha mikakati kupulizia maeneo ya umma kama vile masoko na vituo vya matatu dawa zenye kemikali kuua viini virusi vya corona.

Waziri alisisitiza haja ya watu kuendelea kuvalia maski hasa wakiwa katika maeneo ya umma, akisema uchunguzi umeonyesha mkakati huo unaosaidia kuzuia kusambaa kwa corona unakiukwa na wengi.

“Uvaliaji maski na umbali kati ya mtu na mwenzake umeidhinishwa kusaidia kuzuia msambao wa virusi vya corona,” alieleza. Pia, watu wanahimizwa kunawa mikono kila wakati kwa sabuni au kwa jeli.