Habari Mseto

Korti yamfunga nyanya jambazi miaka 35 jela

August 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

NYANYA wa miaka 62 ambaye amekuwa akishiriki ujambazi kwa miaka mingi amefungwa jela miaka 35 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mabavu. Joyce Wairimu Kariuki alipatikana na hatia ya wizi wa mabavu uliohusisha visa vya unyang’anyi wa magari hasa malori yanayobeba mizigo maeneo ya Nakuru, Mombasa na Nairobi.

Mwanamke huyo ambaye wapelelezi wamemtaja kama kiongozi wa mtandao wa genge la majambazi, alishtakiwa Aprili 23 2019 katika Mahakama ya Loitoktok miezi michache baada ya kuachiliwa kutoka gereza la Shimo la Tewa mjini Mombasa ambako alitumikia kifungo cha miaka 15 na miezi sita kwa kesi nyingine sita za wizi alizotenda maeneo tofuati.

Kushtakiwa kwake Loitoktok kulifuatia uchunguzi ambao ulimhusisha na visa kadhaa vya watu kunyang’anywa magari kaunti za Nakuru, Nairobi na Mombasa kati ya 2018 na Aprili 2019, kumaanisha hakurekebisha tabia licha ya kufungwa jela zaidi ya miaka 15 kwa kesi za awali.

“Kufuatia ripoti za magari kuibwa na hasa malori maeneo ya Nakuru, Nairobi na Mombasa kati ya 2018 na 2019, uchunguzi wa wapelelezi wa DCI katika kesi zote, uliwaelekeza kwa mshtakiwa licha ya kuwa aliachiliwa kutoka gereza la Shimo la Tewa baada ya kukamilisha kifungo cha miaka 15,” DCI ilisema kwenye taarifa.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba mwanamke huyo alifungwa jela kuanzia mwaka wa 2006 baada ya kuhusika na visa vya wizi kaunti za Kilifi, Kwale, Nyeri, Murang’a, Nyahururu na Mombasa.Mnamo Oktoba 16 2006, mahakama ya Kilifi ilimhukumu kufungwa miaka mitatu kwa kosa la wizi, na mwaka uliofuata, mahakama ya Nyeri ilimpata na hatia katika kesi nyingine na kumhujumu kufungwa jela miaka miwili.

Mnamo Novemba 6 mwaka huo, mahakama ya Kigumo kaunti ya Murang’a ilimpata na hatia katika kesi nyingine na kumsukuma jela mwaka mmoja.

Rekodi zake za uhalifu zinaonyesha kuwa mnamo wiki mbili baada ya mahakama ya kesi kuamuliwa Kigumo, mahakama ya Hakimu Mkuu ya Mombasa ilimpata na hatia ya wizi na kumhukumu kufungwa jela miaka miwili.

Kulingana na rekodi za korti, mwaka wa 2008, Wairimu alipatikana na hatia katika kesi aliyoshtakiwa mahakama ya Hakimu ya Nyahururu na akahukumiwa kufungwa jela miaka mitatu.

Mnamo Septemba 23 mwaka huo, akiwa bado gerezani, mahakama ya Hakimu ya Kwale ilimuongezea miaka minne ndani ilipompata na hatia ya wizi. Juhudi zake za kukata rufaa katika kesi hizo ziligonga mwamba Jaji Martin Muya alipoitupilia mbali akisema hangeikubali kwa sababu ilihusu kesi tofauti, zilizoamuliwa na Mahakama tofauti tarehe tofauti.

Katika uamuzi aliotoa Novemba 14 2013, Jaji Muya alisema kwamba rufaa ya Wairimu ilihusu kesi alizoshtakiwa kati ya 2006 na 2008. Baada ya rufaa yake kutupwa Wairumu alikaa jela kwa miaka 15 na miezi sita hadi 2018 alipoachiliwa.

Polisi wanasema waligundua badala ya kuacha uhalifu aliingilia wizi wa mabavu ambao Jumanne wiki hii ulimfanya afungwe jela miaka 35. Mwanamke huyo atakuwa amefungwa jela kwa jumla ya miaka 50 na iwapo hataachiliwa kupitia rufaa atatoka jela akiwa na umri wa miaka 97 Mungu akimjaalia.