Uhuru, Ruto na Mudavadi wamenyania kura za Mlima Kenya
Na MWANGI MUIRURI
Vita vya kimaneno vimechipuka kati ya wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta, William Ruto na Musalia Mudavadi eneo la Mlima Kenya katika msukumano wa kusaka ubabe kwa uchaguzi wa 2022.
Mrengo wa Rais ukiongozwa na naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na wabunge kadhaa ulionya kuwa “Mlima Kenya sio kiwanja cha baba wa mkate (Dkt Ruto) ilihali baba msaka riziki (Uhuru)bado yuko kwa boma.”
Murathe aliambia Taifa Leo kuwa wanaorandaranda huku wakisema kuwa 2022 watavuna kura za Mlima Kenya wanafaa waelewe kuwa ufunguo wa hifadhi ya kura hizo uko na Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga ndani ya mrengo wa Handisheki.
“Rais ndiye sauti ya mwisho kuhusu kura za Mlima Kenya. Akisema tuamke siku ya uchaguzi tukazitupe kwa mto tutapiga foleni kando mwa mito yote ya eneo hili tukazitupe…” akasema.
Kwa mafumbo simulizi na huenmda ikaashiria mwelekeo wa rais Kenyatta kuhusu 2022, Murathe akasema: “Akisema tuzipe Kenneth au Raila, hilo ndilo litakuwa jambo la kutekeleza.”
Kenneth alisema kuwa kuna mrengo wa 2022 ambao Rais anasuka na utakuja kuwashtua wanaojidhania kuwa wamejipa guu mbele Mlima Kenya.
“Rais alitwambia kuwa atatangaza kitu kuhusu 2022 na tutashtuka…Sitaki kuelezea mengi lakini ni vyema ieleweke mapema kuwa Mlima Kenya umefungwa dhidi ya matapeli wa kisiasa ambao licha ya kuwapa nafasi ya kupanda ngazi hadi kuwa manaibu wa Rais, waliingiwa na kiburi na wamekuwa wakiunganisha watundu na watukutu wa kisiasa Mlima Kenya kumdunisha rais,” akasema.
Lakini wakereketwa wa mrenngo wa Dkt Ruto walijibu mipigo wakisema kuwa hawana wasiwasi na matamshi ya Murathe na washirika wao ndani ya Handisheki.
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro pamoja na mwenzake wa Kandara Alice Wahome sambamba na wa Mathira Rigathi Gachagua walisema kuwa kura ziko na raia bali haziko kwa midomo ya hawa wanaoongea kwa vitisho.
Akasema Nyoro: “Ikiwa Murathe na Kenneth na washirika wao wameamua kuwa watampigia Bw Odinga kura, wafanye hivyo bila kelele. Sijui ni kitu gani kinawasumbua. Sisi tuliamua kunyamaza tungoje kalenda ya uchaguzi wa 2022 itimize tarehe tuamke tukamwajibikie Dkt Ruto. Wao hawachoki kutuandama na maneno.”
Gachagua alisema kuwa “shida kuu ya Handisheki ni kufikiria sisi ni wanyama wa kupigiwa debe tupu tuingie mitini kwa uoga. Waje na tutamenyana nao kisawasawa. Mtu mmoja (Dkt Ruto) na wanamwinda wakiwa na kila aina ya silaha na kelele…Ina maana kuwa wanamuogopa si haba.”
Nao washirika wa Mudavadi wakiongozwa na mwenyekiti wa Amani National Congress (ANC) Mlima Kenya Simon Gikuru walisuta mirengo hiyo miwili wakisema “Mlima Kenya sio uwanja wa siasa za ukabila na ubabe wa mtu mmoja.”
Alisema kuwa Mudavadi amejishindia wafuasi wengi eneo hili “na tutawashangaza washirika wa Handisheki kwa kuwa ndio wamezoea kutoa vitisho kwa kila sauti mbadala kuhusu siasa za eneo hili.”
Alisema kuwa mrengo wa Dkt Ruto umekuwa ukikandamizwa na ule wa Handisheki akisema kuwa ikiwa kutakuwa na muungano wa kuwania urais kwa pamoja 2022 eneo hilo, “basi tunaweza tu kujiunga na wanatangatanga wala sio wa Handisheki.”
Ni wazo ambalo liliungwa mkono na aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Pere Kamande aliyesema kuwa “hapa Mlimani sisi tumeamua kuwa na mawazo pana ya kisiasa na hatutaki kujikwamiza katika siasa za kufuata mtu mmoja atuongoze bali demokrasia itapewa nafasi inawili hapa.”
Alisema mrengo wa Handisheki umejaaliwa kiburi cha kutisha wengine, akionya kuwa “watu wa kusukumwa kama kondoo watakuwa wachache sana 2022.”
Hata hivyo, Mutrathe alionya kuwa “hizo ni kelele za chura, wajiandae kutokomezwa na mawimbi ya Handisheki kwa kuwa Rais na Bw Odinga wakiwasha moto wa BBI na umoja wa 2022, Mung tu ndiye atawanusuru hawa walio na macho na masikio lakini wameamua hawataki kuona au kusikia.”