Mwanamume kumlipa mkewe wa zamani Sh127,000 kila mwezi
Na RICHARD MUNGUTI
JUHUDI za mwanaume za kupunguziwa mzigo wa kumtunza na kumpa mkewe aliyemtaliki kitita cha Sh127,000 kila mwezi maisha yake yote hapa ulimwenguni iligeuka kuwa kufukuza kifuli baada ya mahakama ya upeo kumwamuru abebe mzigo wake.
Jaji Mkuu David Maraga pamoja na majaji wengine wanne walimwamuru Charles Michael Angus Walkers Munro aendelee kumlisha vinono mkewe ambaye ndoa yao ilijikwaa kisha wakatalikiana.
Majaji hao walikataa kukubalia ombi la Munro kwamba yeye ama mwanaume mwingine yule aliyetalikiana na mkewe hapasi kumsaidia ama kumtunza ikiwa yuko na mapato.
Lakini majaji hao walikataa na kusema vinono na maisha ya bashasha ambayo mwanaume humzoesha mkewe atavigharamia hadi kifo kitakapowatenganisha.
“Hili ni suala la kijamii linalohusu mtu na mkewe. Hatuna mamlaka kisheria kuingilia na kuvuruga maagizo mume awe akimlipa mkewe kiasi kilichowekwa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama kuu,” walisema majaji watano wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu (CJ) David Maraga.
Uamuzi huo ulitowesha matumaini ya Bw Bw Charles Michael Angus Walkers Munro kupunguziwa gharama za kumtunza mkewe aliyemtaliki.
Pia wanaume wengine waliokuwa wanasubiri kwa hamu na ghamu uamuzi huo ndipo wapunguziwe gharama za kuwatunza wake wao waliowapiga teke ziligonga mwamba.
Jaji Maraga na Majaji Jackton Ojwang , Njoki Ndung’u na Smokin Wanjala walikataa kubatilisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ambapo Bw Munro aliagizwa awe akimtunza mkewe na kumpa vinono alizomzoesha nchini Uingereza na humu nchini.
Majaji hao walisema suala la talaka sio suala la kikatiba bali ni suala la kijamii na “hawana mamlaka kisheria kuvuruga uamuzi uliopitishwa na mahakama ya rufaa na mahakama kuu.”
Majaji hao walisema lazima Bw Munro aendelee kufadhili raha za mkewe waliyetengana.
Bw Munro ambaye ni raia wa Kenya alikuwa amewasilisha rufaa kupinga agizo awe akimlipa mkewe Bi Pamela Ann Walker Munro kitita cha Sh127,000 kila mwezi baada ya kumtaliki.
Bi Pamela Ann ambaye ni raia wa Uingereza alikuwa amefunga ndoa na Bw Munro na ndoa yao haikujaliwa watoto.
Mapato ya juu
Katika rufaa yake, Bw Munro alikuwa amesema mkewe huyo waliyetangana “anaweza kujikimu kimaisha kwa vile alikuwa na mapato ya juu.”
Bw Munro alikuwa amedokeza Pamela Anne alikuwa na nyumba nchini Uingereza na alikuwa anapokea pensheni ya mumewe wa kwanza aliyekuwa afisa wa Kijeshi.
Alisema jumba hilo la kifahari liko ulaya na alilikodisha walipokuwa wanahamia nchini Kenya. Makazi yao humu nchini yalikuwa kaunti ya Kilifi.
Lakini walipotengana mwaka wa 2013 Jaji Christine Meoli aliambiwa Bw Munro alihama na kurudi Uingereza na kumwacha mkewe Kilifi.
Mkewe huyo alimweleza Jaji Meoli mumewe alimwacha kwa upweke na kushikana na wanawake wengine kuponda raha.
Pamela alikuwa ameomba mahakama iamuru Bw Munro awe akimlipa Sh250,000 kila mwezi.
Bw Munro alisema yeye ndiye mume wa pili kumuoa Pamela na kwamba “hastahili kumuongezea pesa juu ya pesa.”
Katika rufaa aliyowasilisha mbele ya Majaji Milton Asike Mahakhandia,William Ouko na Kathurima M’Inoti , Bw Munro alilalamika Sh127,000 alizoagizwa na Jaji Meoli awe akimlipa mkewe ni nyingi zapasa kupunguzwa.
Wakauliza, “Mbona sasa Bw Munro anataka kubanduka ilhali alikuwa amemzoesha mkewe maisha ya juu. Lazima aendelee kumweka katika maisha aliyomzoesha.”
Majaji hao walisema hawatakuwa na utu endapo watabatilisha uamuzi wa Jaji Meoli.
“Ulimzoesha mkeo vinono na maisha ya kifahari, endelea kuyagharamia,” waliamuru majaji hao.