Vigogo wa Nasa wapigana makumbo wakijipendekeza kwa Uhuru
Na BENSON MATHEKA
Rais Uhuru Kenyatta anatabasamu huku viongozi wa vyama vya kisiasa wanaopaswa kuwa wakimulika serikali yake katika upinzani waking’ang’ania baraka zake waweze kumrithi atakapoondoka mamlakani 2022.
Viongozi wa vyama vya ODM, Wiper na Amani National Congress (ANC) ambavyo ni washirika katika muungano wa NASA uliompinga Rais Kenyatta katika chaguzi za 2013 na 2017, wameanza kulaumiana kila mmoja akitaka kuwa karibu na Rais Kenyatta.
Vyama hivyo vinatumia mbinu tofauti za kudhalilishana katika juhudi za kuhakikisha kiongozi wa nchi ataunga mkono juhudi zao kugombea urais 2022.Chama cha ODM, kilichokuwa cha kwanza kujenga ukaribu wa kisiasa na Rais Kenyatta kupitia handisheki yake na Bw Odinga miaka miwili iliyopita, kilikuwa na hakika kwamba kiliwapiga kumbo viongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi wa ANC.
Chama hicho kilikuwa na uhusiano mzuri na Rais Kenyatta na kikadharau hadharani washirika wake katika NASA. Kilitangaza kuwa kingeungana na Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kikavamia eneo la Magharibi kusambaratisha juhudi za Bw Mudavadi kuungana na kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula.
“Kwa kufanya hivi, kilitaka kuhakikisha jamii ya Mulembe imegawanyika ili kunyima Bw Mudavadi ushawishi wa kisiasa kumwezesha kujitetea katika ngazi ya kitaifa,” alisema mdadisi wa kisiasa, Benard Wekesa.
Kiliwavuta baadhi ya wabunge wa ANC upande wake kama mbinu ya kufifisha umaarufu wa Bw Mudavadi. Hata hivyo, Bw Mudavadi alikaa ngumu na kucheza chini akihimili mawimbi na juzi akabadilisha mbinu na kutangaza kuwa atashirikiana na Rais Kenyatta katika juhudi zake za kupigana na ufisadi.
Wakati ODM cha Bw Odinga kilipokuwa kikipambana kummaliza Bw Mudavadi katika ngome yake, Bw Musyoka, ambaye alikuwa amejitwika jukumu la mtu wa mkono wa Rais Kenyatta, alikuwa akicheza chini ya maji kuimarisha ukuruba wake na kiongozi wa nchi.
Mnamo Mei, alitia sahihi mkataba wa ushirikiano na chama cha Jubilee na miezi miwili baadaye, chama chake kikatangaza mipango ya kuungana na Jubilee.
“Hatua hii ililenga kupiku ODM ambacho kimejivuta kutia sahihi mkataba wa ushirikiano na Jubilee. Wiper kilitumia fursa hiyo kujenga imani yake kwa Rais Kenyatta kwamba kina nia njema katika ushirikiano wao wa kisiasa,” asema Bw Wekesa.
Anasema hatua ya Wiper ilishtua ODM na kumlaumu Bw Musyoka kwa kutaka kupindua uhusiano wa chama hicho cha chungwa na Rais Kenyatta. “Hii ndiyo ilimfanya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kumlaumu Bw Musyoka kwa kupindua handisheki ya Bw Odinga na Rais Kenyatta,” alisema Bw Wekesa.
Muda mfupi baada ya Wiper kutangaza mipango ya kuungana na Jubilee, Bw Sifuna alimshambulia Bw Musyoka akimlaumu kwa kuhujumu ODM.
“Kila kitu Bw Musyoka na Wiper wanachofanya, wanalenga kuhujumu ODM, hiyo ndiyo tabia yao,” Bw Sifuna alinukuliwa akisema. Kulingana na Bw Sifuna, Wiper inafikiria kwamba kwa kukimbia kuungana na Jubilee, watakuwa wenyeji wa ODM katika handisheki kwa sababu itakuwa upande wa serikali jinsi kilivyofanya chama cha Kanu.
Hata hivyo, Naibu Mwenyekiti wa Wiper Victor Swanya anasema chama hicho hufanya maamuzi kwa njia ya wazi kwa lengo la kujiimarisha. Alilaumu ODM kwa kutaka kuwekea Wiper visiki kisiungane na Jubilee kumsaidia Rais Uhuru kuafikia malengo yake ya kuunganisha Wakenya.
“Kama kuna chama kinachotaka kuzima ajenda ya Rais Uhuru, basi ni ODM, sio Wiper. ODM hakiwezi kudai kimejitolea kuunganisha nchi huku kikipiga vita washirika wake wanapoungana na rais,” Bw Swanya alisema.
Kulingana na mdadisi wa Siasa Geoffrey Ochoki, ODM kilikosea kwa kudharau vyama tanzu vya muungano wa NASA na kumwamini Rais Kenyatta.
“Viongozi wa chama cha ODM walisahau kuwa siasa ni telezi, wakajipiga kifua na kudharau vyama tanzu katika NASA kwa sababu kina idadi kubwa ya wabunge. Kilisahau kwamba uchaguzi wa 2022 hautajali idadi ya wabunge kilicho nao kwa sasa na kwamba Rais Kenyatta ana malengo yake pia,” alisema.
Mdadisi huyo anasema kwamba mbinu za chama hicho zimevurugika baada ya Bw Mudavadi kutangaza kuwa anaunga Rais Kenyatta na hata akapenya eneo la Mlima Kenya na kuungwa mkono na makundi ya wanasiasa.
“Mbinu ya ODM eneo la Magharibi ilikuwa kwamba Mudavadi haungi Mpango wa Maridhiano (BBI) kikamilifu. Sasa amewapiga kumbo kwa kumuunga Rais Kenyatta,” asema.
Wadadisi wanasema kwamba japo hatua ya Bw Mudavadi ya kubadilisha nia inaweza kuchangiwa na presha na vitisho ndani ya chama chake, alikuwa akizungumza chini kwa chini na Naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe ambaye ni rafiki yake wa miaka mingi.
“Hii inaonyesha kuwa Rais Kenyatta anatabasamu tu viongozi wanaopaswa kuwa wakimulika utawala wake, wakipigana kila mmoja akitaka amuunge mkono 2022,” asema.