WHO yatoa msaada wa magari kuhamasisha umma kuhusu corona
Na DIANA MUTHEU
SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limetoa msaada wa magari sita kwa kaunti ya Mombasa yatakayotumika kuhamasisha wananchi kuhusu virusi vya corona.
Magari hayo yana vipaza sauti na maneno ya kuhamasisha wakazi kuchukua tahadhari kama vile; tuzijue hali yetu, tuoshe mikono kwa sabuni na mengine yameandikwa ili ujumbe uwafikie wakazi wote.
Akizungumza na Taifa Leo wakati wa kuzindua magari hayo nje ya ofisi za kaunti hiyo, Afisa Mkuu wa Afya ya Umma, Bi Aisha Abubakar alisema kwa ushirikiano na shirika la The United Front, watabadilisha mtindo wa mawasiliano kuhusu janga hili kwa kuwa baadhi ya watu wanaendelea kupuuza hatua zilizowekwa kuzuia maambukizi ya maradhi ya Covid-19.
Bi Abubakar alisema kuwa wagonjwa wengi waliopatikana na maradhi hayo hawakuonyesha dalili zilizoorodheshwa hapo awali, na hivyo ni wajibu wa serikali hiyo kutafuta mbinu rahisi ya kuwaelimisha wakazi kuhusu virusi hivyo, kwa undani.
“Baadhi ya wagonjwa waliopatikana na virusi hivyo walikana kwa kuwa hawakuweza kupata dalili zilizoorodheshwa hapo mwanzoni. Ni jukumu letu kama wizara kuwaelimisha wanajamii kuhusu maradhi haya na ni hatua gani wanafaa kuchukua kujilinda,” akasema Bi Abubakar.
Wizara ya Afya katika kaunti hiyo ilisema kuwa zaidi ya watu 37,000 wameweza kupimwa corona na walioambukizwa ni 2200 kufikia jana.
Katika kaunti hiyo, eneobunge la Mvita ndilo linaongoza kwa idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona, wagonjwa hao wakiwa 774.
Bi Abubakar alisema tayari wanaendelea na shughuli za kuhamasisha umma katika maeneo bunge ya Kisauni, Jomvu na Changamwe kwa ushirikiano na mashirika ya kijamii.
Mwenyekiti wa afisa wa shirika la The United Front, Bw Said Mabruk alisema kuwa katika kila gari kutakuwa na afisa wa afya ya umma atakayezungumza na wakazi, na pia kuyajibu maswali watakayouliza kuhusiana na virusi vya corona.
“Tunataka wakazi wote wapate ujumbe mwafaka kutoka kwa wataalamu. Pia, tunalenga kuwapa mafunzo zaidi ya watu 1000 watakaotusaidia kuhamasisha wakazi wa Mombasa kuhusu janga hili,” akasema Bw Mabruk.