HabariSiasa

ODM yajitosa kwa kashfa ya Sh9 bilioni NYS

May 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

ERIC WAINAINA na MERCY KOSKEY

CHAMA cha ODM Jumatatu kilijitosa kwenye kashfa ya mabilioni ya pesa katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS) kikitaka wahusika wa wizi wa mabilioni wakabiliwe vikali.

Hii ni kufuatia ufichuzi wa gazeti Daily Nation kuwa Sh9 bilioni zimeibwa kutoka NYS kupitia mpango uliohusisha kuvurugwa kwa mtambo wa IFMIS, ambao hutumika katika utoaji wa kandarasi na malipo yake.

Kupitia mpango huo ambao unaaminika kuhusisha maafisa wa ngazi za juu serikalini, Sh9 bilioni zimeibwa tangu 2016. Hii ni sakata ya pili kubwa ya wizi wwa mabilioni ya pesa katika NYS. Maafisa wakuu wa katika idara hiyo wamehojiwa huku kampuni kadhaa zikimulikwa.

Hapo Jumatatu, ODM kilisema hata kama Bw Raila Odinga aliweka muafaka na Rais Uhuru Kenyatta, hawatasita kuendeleza shinikizo dhidi ya maafisa wa serikali wanaojihusisha na ufisadi.

“Hatutakaa kitako kutazama watu wakifuja rasilimali za nchi hii. Tunataka kutoa wito kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na Idara ya Upelelezi wa Jinai ziharakishe uchunguzi na wahusika wapelekwe mahakamani kujibu mashtaka kwa sababu ni lazima sakata hizi za ufisadi zikome,” akasema Katibu Mkuu, Edwin Sifuna.

Ripoti zinasema DCI inachunguza kampuni 36 zinazoshukiwa zilifaidika na ufujaji wa pesa hizo.

“Iwe ni wanachama wa ODM au wa chama chochote kingine, sisi kama chama hatutamlinda mtu yeyote ambaye anajihusisha na ufisadi. Kwanza tutawafurusha watu wa aina hiyo chamani kwa sababu tunajaribu kujenga taifa hili,” akasema Bw Sifuna.

Aliongeza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni mojawapo ya makubaliano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga katika juhudi zao za kuleta mabadiliko ya kuendeleza taifa mbele.

Katika miaka iliyopita, sakata nyingi za ufisadi zilizofichuliwa zilifanyiwa uchunguzi lakini washukiwa wengi waliotajwa, hasa wenye ushawishi mkubwa serikalini huachiliwa huru kutokana na kisingizio cha ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuwapata na hatia.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Mohammed Haji jana alisema afisi yake itafanya kila juhudi kushtaki washukiwa wa ufisadi bila kujali misimamo yao ya kijamii, kiuchumi wala kidini.

Katika sakata kubwa ambazo zimewahi kushuhudiwa nchini washukiwa wangali huru.