Habari Mseto

Kanisa Katoliki lapinga refarenda ya kujali wachache

August 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

KANISA Katoliki limewataka Wakenya kukataa jaribio la kutaka kurekebisha Katiba kwa manufaa ya wanasiasa wachache.

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (KCCB), jana lilisema kuwa shughuli ya kuandaa kura ya maamuzi ni ghali mno hivyo haifai kuendeshwa kuwanufaisha wanasiasa wachache.

Mchakato wa kurekebisha katiba unapigiwa debe na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Badala yake, baraza hilo liliwataka viongozi wa kisiasa kuelekeza juhudi zao katika kufufua uchumi uliodorora kufuatia janga la virusi vya corona.

Maaskofu hao walionya kuwa kura ya maamuzi huenda ikagawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila kama ilivyoshuhudiwa 2005 na 2010.

“Wakati wa kura ya maamuzi ya kubadili katiba ya 2005 na 2010, kulikuwa na mgawanyiko mkubwa nchini. Hivyo tunafaa kuepuka migawanyiko sawa na hiyo kwa sasa.

“Vilevile, kura ya maamuzi itasababisha nchi kupoteza fedha nyingi ambazo zinafaa kutumiwa kukwamua hali ya maisha ya Wakenya na uchumi ambao umeathiriwa pakubwa na janga la corona,” ikasema taarifa yao iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa KCCB, Askofu Philip Anyolo.

Walihimiza Wakenya kukubali kufanyika kwa kura ya maamuzi ikiwa tu mabadiliko hayo yatakuwa ya muda mrefu na manufaa kwa wananchi wote.

“Ikiwa mabadiliko hayo ya katiba ni ya muda mfupi na yanalenga kuwanufaisha wanasiasa wachache kwa maslahi yao ya kibinafsi, basi Wakenya wakatae,” akasema Askofu Anyolo.

Wakuu hao wa Kanisa Katoliki walitoa tamko lao huku kukurukakara za kutaka kurekebisha katiba kupitia kura ya maamuzi zikiwa zimeanza kushika kasi baada ya kukatizwa kwa mikutano iliyopita kufuatia janga la virusi vya corona.

Rais Kenyatta katika hotuba yake kwa taifa wiki iliyopita, alisema kuwa wakati umewadia wa kubadili katiba iliyopitishwa na Wakenya miaka 10 iliyopita.

Naye Bw Odinga anashikilia kuwa kura ya maamuzi kurekebisha katiba itafanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.Jopokazi la BBI lililobuniwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya lilikamilisha ripoti yake ya mwisho Juni 30, mwaka huu, na inatarajiwa kukabidhiwa kwa viongozi hao wawili wakati wowote.

Ripoti ya kwanza ya BBI iliyozinduliwa mnamo Novemba, mwaka jana, ilipendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu atakayekuwa na manaibu wawili.

Ripoti hiyo pia ilipendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa kiongozi wa upinzani.

Japo yaliyomo katika ripoti ya mwisho hayajawekwa wazi, mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, jana alidokeza kuwa inapendekeza kuwa rais awe na manaibu wawili.Kulingana na Bw Murathe, Rais Kenyatta ataunga mkono Bw Odinga kuwania urais na Seneta wa Baringo Gideon Moi na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, watakuwa manaibu wake.

“Tunafaa kujiuliza ikiwa mambo hayo yanayopendekezwa kubadilishwa ni ya dharura na yatanufaisha hata vizazi vijavyo. Ikiwa hakuna dharura yoyote hakuna haja ya kuwa na kura ya maamuzi,” wakasema makasisi hao.

Wakati huo huo, viongozi hao wa Kanisa Katoliki waliwataka wanasiasa ambao sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2022 kutochochea uhasama wa kikabila nchini.

“Kujipanga kwa wanasiasa uchaguzi unapokaribia ni jambo la kawaida. Lakini hicho kisiwe kisingizio cha kuchochea uhasama wa kikabila,” akasema Kasisi Anyolo.

Walizitaka taasisi za kupambana na ufisadi kuchunguza madai ya wizi wa fedha zilizotengwa kupambana na janga la virusi vya corona.