Habari Mseto

Je, maji haya yatapunguza gharama ya umeme?

May 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Bei ya umeme inatarajiwa kushuka zaidi katika muda wa miezi kadhaa ijayo kutokana na ongezeko la kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme nchini.

Tangu 2015, kiasi cha sasa cha maji katika mabwawa hayo ndicho cha juu zaidi. Waziri wa Kawi Charles Keter Jumanne alisema viwanda vya kuzalisha umeme katika Mto Tana vina maji mengi zaidi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini.

Hii ni kumaanisha kuwa gharama ya matumizi ya umeme itapungua kwa watu binafsi na kampuni.

Kwa sasa, kiwango cha umeme unaotolewa kwa kuzalishwa na maji ni asilimia 40. Alisema hayo saa chache baada ya serikali kutangaza mpango wa kuondoa baadhi ya ada katika matumizi ya umeme nchini.

“Tuko sawa hadi Desemba,” alisema Keter na kukanusha hofu kwamba huenda gharama ya kununua stima ikaongezeka.

Lakini hadi Wakenya wajionee ukweli wa maneno yake katika muda wa miezi ijayo kwani awali kumekuwa na ahadi za kupunguza gharama ya umeme huku ikizidi kupanda.