Michezo

Bale kukosa mechi tano zijazo za Tottenham kwa sababu ya jeraha

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

FOWADI Gareth Bale, 31, amewataka mashabiki wa Tottenham Hotspur kutarajia makuu kutoka kwake msimu huu baada ya kufichua kwamba ana kiu na motisha ya kutwaa mataji zaidi akiwa nao.

Spurs walimsajili Bale kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Real Madrid mnamo Septemba 19, 2020.

Nyota huyo raia wa Wales aliagana na Spurs mnamo 2013 baada ya kusajiliwa na Real kwa kima cha Sh11 bilioni. Akiwa Real, alifunga zaidi ya mabao 100 na kusaidia kikosi hicho kutwaa mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Najihisi vizuri kurejea. Spurs ni klabu spesheli sana kwangu. Ndipo nilipojijengea jina kitaaluma,” akatanguliza Bale.

“Natarajia kujinyanyua haraka iwezekanavyo na kusaidia Spurs kurejea wanakostahili kuwa na kuwanyanyulia mataji ya haiba chini ya kocha Jose Mourinho,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Spurs, Bale amejiunga nao akiwa na jeraha la goti alilolipata wakati akichezea Wales mwanzoni mwa Septemba 2020.

“Tutaanza kumchezesha baada ya likizo fupi ya Oktoba itakayopisha mechi za kimataifa. Tunatarajia kwamba atakuwa amepona jeraha kufikia wakati huo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Spurs.

Ina maana kwamba Bale atakosa jumla ya mechi tano zijazo za Spurs na gozi la kwanza atakalolisakata ndani ya jezi za waajiri wake ni dhidi ya West Ham mnamo Oktoba 17, 2020.

Bale alisajiliwa na Spurs kwa mara ya kwanza mnamo 2007 kwa kima cha Sh700 milioni. Mbali na kunyanyua mataji manne ya UEFA akiwa Real, pia alisaidia miamba hao wa soka ya Uhispania kutwaa makombe mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na mataji matatu ya Kombe la Dunia.

Bale anasalia kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza na ndiye Mwingereza (Wales) anayejivunia kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya Uhispania. Anajivunia kuwafungia Real jumla ya mabao 80 na kuchangia mengine 40 katika jumla ya mechi 171 zilizopita.

Kiini cha kubanduka kwake Real ni kudorora kwa uhusiano kati yake na kocha raia wa Ufaransa, Zinedine Zidane.

Kwa kumsajili Bale kwa Sh11 bilioni, Real walivunja rekodi ya Sh10.8 bilioni walizoweka mezani mnamo 2009 kwa minajili ya huduma za nyota raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo mnamo 2009.

Katika mkataba wake wa kwanza wa miaka sita, Bale alikuwa akilipwa na Real mshahara wa Sh42 milioni kwa wiki kabla ya kutia saini mkataba mwingine wa miaka sita mnamo 2016 ambapo alikuwa akilipwa Sh84 milioni kwa wiki.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO