• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
RUTO AMNYIMA RAILA USINGIZI

RUTO AMNYIMA RAILA USINGIZI

Na VALENTINE OBARA

HATUA zinazochukuliwa na Naibu Rais William Ruto kujikuza kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 zimeonekana kuzindua chama cha ODM.

Chama hicho kikiongozwa na Bw Raila Odinga sasa kimeamua kubuni mikakati ya kukabiliana na mipango yote inayoendelezwa na Dkt Ruto anayepanga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kustaafu kikatiba baada ya kukamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi.

Ijapokuwa Bw Odinga hajatangaza wazi kama atawania urais kwa mara nyingine, ODM haijaficha kwamba kitakuwa na mgombeaji katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mnamo Jumamosi, chama hicho kilikamilisha mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) katika Kaunti ya Machakos, ambapo ilibainika kuwa mengi yaliyojadiliwa yalihusu mbinu za kuzuia ODM kufifishwa na makombora ya kisiasa yanayotoka kwa Naibu Rais na wandani wake wa kikundi cha Tangatanga.

Kwa miezi kadhaa sasa, Dkt Ruto amekuwa akiendeleza ziara na mikutano ya kujitafutia umaarufu kila pembe ya nchi hata wakati ambapo mikutano ya kisiasa ilikuwa imepigwa marufuku kwa sababu ya janga la corona.

Katika muda wa tangu Machi ambapo viongozi wengine wa kisiasa walitulia wakisubiri maambukizi ya corona yapungue na nchi ifunguliwe tena, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanahoji kuwa Dkt Ruto alipata nafasi bora ya kupenya katika maeneo tofauti nchini ikiwemo ngome za kisiasa za Bw Odinga.

Masuala ambayo Naibu Rais alivumisha ambayo yalizidisha uhasama kati yake na Bw Odinga ni kama vile kupinga marekebisho ya katiba yanayotarajiwa kuletwa na Mpango wa Maridhiano (BBI), wito wa umoja wa walala-hoi (hasla) dhidi ya mabwanyenye, uchunguzi kuhusu sakata ya ununuzi wa vifaa vya corona katika Mamlaka ya Usambazaji Dawa nchini (KEMSA) na hivi majuzi, mpango wa awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba.

Dkt Ruto amekuwa akikutana na viongozi wenye ushawishi katika jamii kama vile viongozi wa kidini na makundi ya vijana ambapo huwahimiza kuhusu misimamo yake kwa masuala hayo.

Imefichuka kuwa, ODM sasa imepanga kuanzisha vuguvugu kwa jina People’s Power Project (PPP) ambalo litalenga kuvuruga mipango ya Naibu Rais kama vile kuhusu marekebisho ya katiba.

Kwenye mpango huo, ODM imenuia kuimarisha matawi yake kote nchini ili kuepusha wafuasi wake kuyumbishwa.

Hatua hii imetokea wakati ambapo Dkt Ruto tayari amefanikiwa kubuni makundi ya vijana katika ngome za Bw Odinga za kisiasa ikiwemo Kisumu, ambapo baadhi ya wanachama waliadhibiwa hivi majuzi na ODM kwa kuhudhuria mikutano ya wandani wa Naibu Rais.

Mbali na kuzuia wafuasi wake kuyumbishwa, ODM inalenga pia kuingiza viongozi waliokuwa mstari wa mbele kupigania mageuzi zamani, pamoja na mashirika ya kijamii. Kabla ya mkutano wa NEC uliokamilika Jumamosi, Bw Odinga alikuwa tayari ameanzisha mikutano na viongozi wa chama chake mashinani kwa nia ya kukiimarisha.

“Lazima tufikishe ujumbe kwa wananchi kwamba mabadiliko tunayopigania ni kwa manufaa ya taifa na yatatoa nafasi ya ustawi kwa kila mmoja. Lazima tukabiliane na wapinzani wetu na tutoe changamoto kwao kueleza wazi msimamo wao kuhusu wanachotakia nchi na jinsi wanavyolenga kutimiza maazimio yao kwa taifa,” akasema Bw Odinga.

Viongozi wa ODM hueleza wazi kutoridhishwa kwao na jinsi Dkt Ruto na wandani wake wanavyotoa ufadhili wa vifaa vya mamilioni ya pesa kwa makundi ya vijana mara kwa mara.

Bila kumtaja, Bw Odinga alisisitiza kuwa fedha zinazotumiwa kwa ufadhili huo ni za kutiliwa shaka huku akionekana kudai ni mapato yanayotokana na ufisadi.

“Lazima tusione haya wala kuondoa mawazo yetu kwa juhudi za kukuza taifa lililostawi kiuchumi ambalo linaondoa umaskini, ukosefu wa usawa na kuleta nafasi za ajira kwa vijana wetu. Ili kufanikisha malengo haya yote, lazima tujitolee kikamilifu bila uoga katika vita dhidi ya ufisadi. Ufisadi ndio chanzo kikuu cha umaskini ambao unakumba wananchi wetu,” akasema Bw Odinga.

Akisisitiza, alisema, “Katika miezi ijayo, tutaingia katika makabiliano na watu walionufaika kwa mapato ya ufisadi ambao wanapinga ajenda yetu ya mageuzi makuu ya kiuchumi na kijamii, uzalishaji nafasi za ajira na usawa katika ugavi wa rasilimali.”

Dkt Ruto hupuuza wapinzani wake ambao humkashifu kwa utoaji misaada.

Mipango ya ODM/Raila:

  • Kustawisha matawi ya chama ili wafuasi wasiyumbishwe
  • Kutafuta ushirikiano wa mashirika ya kijamii na watetezi wakongwe wa mageuzi
  • Kuandaa msururu wa mikutano na viongozi mashinani ili watetee misimamo ya chama
  • Kuanzisha vuguvugu la mageuzi

You can share this post!

Wauguzi Embu wasitisha mgomo

Madaktari waonya dhidi ya kufungua shule haraka