Kocha Frank de Boer apoteza mechi yake ya kwanza akidhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi
Na MASHIRIKA
KOCHA Frank de Boer alipoteza mechi yake ya kwanza akiwa kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi.
Hii ni baada ya mshambuliaji wa Wolves, Raul Jimenez kufungia Mexico bao la pekee na la ushindi dhidi ya Uholanzi kupitia penalti kwenye mechi ya kirafiki iliyowakutanisha mnamo Oktoba 7, 2020.
Jimenez alipoteza nafasi nyingi za wazi kwenye mchuano huo kabla ya kupata penalti baada ya kuchezewa visivyo na beki matata wa Manchester City, Nathan Ake.
Uholanzi walionekana kuzidiwa maarifa na Mexico katika takriban kila idara kwenye mechi hiyo. Jaribio la pekee lililofanywa na kikosi cha De Boer langoni pa wapinzani ni kupitia kwa mvamizi Memphis Depay aliyeshuhudia kombora lake likibusu mwamba wa goli mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Uholanzi kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Bosnia kwenye mechi ya Uefa Nations League mnamo Oktoba 11, 2020 kabla ya kuchuana na Italia katika kivumbi hicho mnamo Oktoba 14, 2020.
De Boer ambaye ni kocha wa zamani wa Crystal Palace katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alipokezwa mikoba ya kunoa timu ya taifa ya Uholanzi mnamo Septemba 23, 2020 baada ya kuaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa mkufunzi Ronald Koeman aliyeyoyomea Uhispania kudhibiti mikoba ya Barcelona katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 alipokezwa mkataba wa miaka miwili ambao utatamatika mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.
De Boer aliwahi kuwajibishwa katika jumla ya mechi 112 akivalia jezi za Ajax, Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi.
Amewahi pia kuwatia makali vijana wa Inter Milan nchini Italia na Atlanta United katika Major League Soccer (MLS) nchini Amerika kati ya Disemba 2018 na Julai 2020.
De Boer ndiye alikuwa kocha msaidizi wa Uholanzi kikosi hicho kilipotinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini chini ya ukufunzi wa Bert van Marwijk.
Akiwanoa Ajax kati ya Disemba 2020 na Mei 2016, aliongoza kikosi hicho kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Uholanzi.