• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Madereva wa malori wakashifu Macharia

Madereva wa malori wakashifu Macharia

DENNIS LUBANGA na BRIAN OJAMAA

MADEREVA wa matrela wanaosafirisha bidhaa katika nchi za Uganda na Rwanda, wamemlaumu vikali Waziri wa Uchukuzi James Macharia kwa kukosa kushughulikia tatizo la msongamano katika mpaka wa Malaba.

Msongamano huo unakisiwa kufikia umbali wa kilomita 80.

Wakiwahutubia wanahabari mjini Malaba jana, madereva hao walimkashifu vikali Bw Macharia kwa kutozuru eneo hilo tangu janga la Covid-19 kutua nchini mwezi Machi.

“Kwa miezi sita au saba iliyopita msongamano huu umekuwa ukiongezeka kila kuchao. Malalamishi yetu ni kwa sababu serikali ya Kenya imekosa kuingilia kati suala hili.

“Tunashangaa ikiwa hatuna mchango wowote katika ustawi wa nchi; Bw Macharia haonekani kutujali hata kidogo,” akalalama Bw Silas Mathews.

Bw Mathews ambaye husafirisha vyuma kutoka Mombasa hadi mjini Fort Portal, Uganda, alisema madereva wa kusafirisha bidhaa wamekuwa wakiteseka sana tangu janga la Covid-19 kutua nchini.

“Tuliambiwa msongamano huu ulikuwa ukisababishwa na janga. Wenzetu waliokuwa wamekwama waliruhusiwa kwenda na hali ilirejea kama kawaida. Baadhi yetu tumekuwa tukihangaishwa na mamlaka za Uganda bila kupata usaidizi wowote kutoka kwa serikali yetu ya Kenya,” akaongeza.

Alisema raia wa Uganda wanawalaumu kwa kusambaza Covid-19 licha yao kupimwa mara kadhaa kabla kuruhusiwa kuvuka mpaka kuingia taifa hilo jirani.

“Kuna shida kubwa mjini Malaba. Tunamtaka waziri aje hapa na maafisa wake wote ili kutafuta suluhisho la kudumu. Hapaswi kuendelea kukaa ofisini Nairobi mambo yakizidi kuharibika hapa.

“Tena akome kulaumu madereva eti ndio chanzo cha msongamano na usambazaji wa Covid-19,” akaeleza Bw Nicholas Ouma ambaye pia ni dereva.

Alisema kwamba hakuna dereva angetaka kusababisha msongamano huo kimakusudi, kwani lengo la kila mtu ni kufikisha mzigo wake haraka na kuchangamkia kazi nyingine.

“Msongamano huu umeletwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) mpakani. Ajali nyingi zimetokea kwa sababu tu ya hali hii,” akaeleza Bw Ouma.

Dereva mwingine Mohamed Shukri alisisitiza kuwa wanataka kukutana na mawaziri wa uchukuzi wa nchi hizo mbili za Kenya na Uganda ili kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu mkwamo huo.

Alilalamika kwamba takriban madereva 4,000 wamekwama eneo hilo kwa sababu ya kujikokota kwa maafisa wa Uganda kuwapa matokeo ya vipimo vya virusi vya corona, ambavyo ndivyo vinasababisha Covid-19.

“Tunachotaka ni wazir ashauriane na mwenzake wa Uganda ili tuondoe mkwamo huu. Tunalaumiwa kwa kusambaza corona ilhali hakuna hata mmoja wetu amefariki,” akasema Bw Shukri.

You can share this post!

IG atetea polisi wavunjao mikutano ya kisiasa

Wafuasi wa Ruto wasema hawatatishika