AFYA: Ngoja ngoja ya miezi tisa kaja na majonzi tele
NA PAULINE ONGAJI
Ni mwezi mmoja sasa tangu kumpoteza mwanawe na Fatuma Ibrahim, 27, bado anauguza jeraha lililotokana na upasuaji aliofanyiwa wakati huo.
Lakini licha ya kuwa kidonda kingali kibichi, hana budi kuendelea na shughuli yake ya kila siku ya uuzaji mboga ama ukipenda mama mboga.
Kwa Bi Ibrahim, Septemba 4, 2020 itasalia daima kwenye kumbukumbu zake.
Matumaini ya mkazi huyu wa eneo la Bura, Hola, Kaunti ya Tana River kwamba ngoja ngoja yake ya miezi tisa ya ujauzito ingemtunuku zawadi ya mtoto, yaligeuka kilio na majonzi tele moyoni.
“Nilianza kukumbwa na uchungu wa uzazi na nikaenda hospitalini. Niligundua kuna tatizo nilipoumwa kwa muda mrefu sana,” aeleza.
Alipofika hospitalini, kwa saa kadhaa madaktari walishindwa kumzalisha, suala ambalo hatimaye liliwalazimu kumrarua ukeni katika harakati za kumuondoa mtoto ambaye alikuwa amefika kwenye lango la uzazi tayari kutoka.
“Naam niliraruliwa ukeni na mtoto kuondolewa, lakini kwa bahati mbaya alifariki saa moja baadaye. Kulingana na madaktari, mtoto huyo alikuwa amekawia sana kwenye lango la uzazi, akakosa hewa na alikuwa amechoka pia,” aeleza.
Ni tukio lililomsababisha Bi Ibrahim kuvuja damu nyingi na hata kuzimia kwa saa kadhaa pindi baada ya kujifungua.
Haya sio masaibu ya kwanza ya aina hii kumkumba Bi Ibrahim. Mama huyu wa watoto watatu, amekuwa na shida ya kujifungua kila wakati.
Ni shida aliyokumbana nayo mwanzoni miaka 12 iliyopita akijifungua mtoto wake wa kwanza.
“Nakumbuka nilikumbwa na uchungu wa uzazi kwa siku saba ambapo hatimaye nilipojifungua, tayari mtoto alikuwa amechoka na alipozaliwa ikathibitishwa baadaye kwamba alikuwa na utindio wa ubongo (cerebral palsy),” aeleza.
Hii ndio hatima ya wanawake wengi katika jamii nyingi ambazo bado zinahimiza desturi ya ukeketaji katika Kaunti ya Tana River.
“Ukitembea katika kila boma kijijini humu, lazima ukumbane na hadithi ya kutisha kumhusu mwanamke aliyejifungua. Yaweza kuwa ni mama aliyefariki akijifungua, aliyempoteza mwanawe wakati wa kujifungua, au aliyepata nasuri ya uzazi kutokana na matatizo ya kujifungua,” aeleza.
Bi Ibrahim anatoka katika jamii ya Wardey ambayo bado inaendeleza utamaduni huu.
Ukeketaji
Jamii hutekeleza ukeketaji wa aina ya tatu yaani infibulation, ambapo sehemu zote zinazounda uke ikiwa ni pamoja na kinembe, mdomo wa uke na mrija wa mkojo (urethra), hukatwa na kuondolewa kabisa kabla ya sehemu iliyoachwa wazi kuzibwa na kuacha nafasi ndogo ya kupitisha mkojo na damu ya hedhi.
Ni shughuli inayosababisha uchungu usiomithilika sio tu wakati huo wa kukeketwa, bali pia baadaye wakati msichana anapoanza kushuhudia hedhi au wakati wa tendo la ndoa.
“Shimo linaloachwa huwa ndogo sana ambapo lazima lipanuliwe tena kwa kukatwa kwa wembe au kisu, ili mwanamume aweze kupenya wakati wa tendo la ndoa,” aeleza Nastehe Abubakar, mwanaharakati dhidi ya ukeketaji na mratibu wa chama cha Dayaa Women Group.
Hata hivyo ni madhara ya afya kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua ndio yameonekana kuwa mabaya zaidi kutokana na ukeketaji.
Kulingana na Dkt Oscar Endekwa, Mkurugenzi wa masuala ya afya katika Kaunti ya Tana River, mambo huwa mabaya hata zaidi wakati wa kujifungua ambapo lazima uke ukatwe tena, suala ambalo laweza msababishia mama na mtoto matatizo ya kiafya wakati huu,” aeleza.
“Wakati wa uchungu wa uzazi, jukumu la daktari ni kumkagua mama na mtoto. Ukaguzi huu hufanyika hasa kupitia lango la uzazi, na ikiwa sehemu hii imezibwa kutokana na ukeketaji, basi inakuwa vigumu kufanya hivyo,” aeleza.
Pia, Dkt Endekwa asema kutokana na sababu kwamba lango la uzazi limezibwa, kuna uwezekano mkubwa wa sehemu hii kuraruka, na hivyo kusababisha maumivu makuu wakati wa kujifungua.
Kulingana na Bi Abubakar, ni sababu hii ambayo imefanya wanawake wengi katika eneo hili kuhofia kwenda hospitalini wanapotaka kujifungua. “Wengi wanahofia kwamba wakienda hospitalini, madaktari watalazimika kurarua uke kwa makasi, kumtoa mtoto kisha kushona tena. Hii husababisha maumivu ambayo hutisha hata zaidi wakati wa kujifungua mtoto mwingine, kwani jeraha hilo litakatwa tena,” aeleza.
“Wengi wanaonelea afadhali kwenda kwa mkunga wa kienyeji kukatwa sehemu hii kwa wembe na kuzibwa kwa njia za kiasili, ambapo wakati wa kujifungua kwa mara nyingine, hatalazimika kushonwa,” aongeza.
Ni dhana ambayo hata hivyo imekuwa na madhara mengi kwa akina mama wa sehemu hii, ambapo hofu hii yao mara nyingi imewasababisha kufika hospitalini wakiwa wamechelewa.
Kulingana na Dkt Endekwa, ni 50% pekee ya akina mama eneo hili wanaotumia huduma za mhudumu wa kiafya aliyehitimu wakati wa kujifungua, huku wengi wakiamua kujifungua mikononi mwa wakunga wa kienyeji.
Dkt Endekwa asema kwamba wengi wa akina mama huvumilia maumivu wakiwa nyumbani na wanapozidiwa na kuamua kwenda hospitalini, tayari afya ya mama na mtoto huwa hatarini.
“Kwa yule ambaye ashajifungua na kukatwa, kuna hatari ya maambukizi kwani vifaa vilivyotumika kufanya kazi hii sio vya kitaalamu na havijatibiwa. Aidha lazima majeraha hayo yashughulikiwe na kutibiwa kitaalamu, shughuli ambayo yaweza fanywa tu hospitalini” anasema.
Pia, Dkt Endekwa asema kwamba hatari kubwa hapa ni kwamba mama atavuja damu nyingi, kichocheo kikuu cha vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” aeleza.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani, idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya kujifungua, iko juu katika mataifa ambapo bado ukeketaji unaendelezwa.
Kwa mfano, kwa mujibu wa ripoti ya kiafya iliyochapishwa miaka miwili iliyopita, eneo la Mandera lilikuwa na idadi kubwa ya vifo vya akina mama kutokana na matatizo wakati wa kujifungua, kuliko sehemu yoyote nyingine ulimwenguni.
Vifo
Uchunguzi wa kiafya ya KDHS; KNBS and ICF Macro uliozinduliwa mwaka wa 2010 ulionyesha kwamba bado idadi ya wanawake wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua kutokana na sababu ambazo zaweza zuiwa kama vile njia ya uzazi kuziba, tatizo ambalo hasa husababishwa na ukeketaji, ingali iko juu.
Lakini kando na matatizo wakati wa kujifungua, Dkt Endekwa asema kwamba, kuna matatizo mengine ya kiafya yanayotokana na utamaduni huu.
Vile vile asema matatizo mengine ya uzazi yanayotokana na ukeketaji yanayoshuhudiwa sana sehemu hii ni kama vile nasuri ya uzazi au mtoto kukumbwa na utindio wa ubongo.
“Wakati wa kujifungua, sharti kibofu kiondolewe mkojo ambapo ikiwa mwanamke amefanyiwa ukeketaji wa aina ya tatu, inakuwa vigumu kufikia mrija wa mkojo, ambapo mwanamke atakumbwa na uchungu wa uzazi akiwa na mkojo. Hali hii inaunda mazingira mwafaka kwa nasuri ya uzazi kutokea,” aeleza.
Wakati huo huo, Dkt Endekwa anasema kwamba suala la unyanyapaa katika eneo hili, limetatiza juhudi za kutambua na kudhibiti mapema nasuri ya uzazi na utindio wa ubongo.
“Pia, kuna wanawake kutoka vijiji vya mbali ambao hawawezi fika hospitalini mapema. Na kuna wahusika wanaojificha na kuficha watoto, na kutatiza juhudi za kakabiliana na tatizo hili,” asema.