• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Maafisa wa ardhi kuhamasisha wakazi wa Thika

Maafisa wa ardhi kuhamasisha wakazi wa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

ULAGHAI wa uuzaji na ununuzi wa vipande vya ardhi katika mji wa Thika umezidi huku wakazi wake wakitaka hali hiyo kuthibitiwa.

Hata hivyo, mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amesema wamefanya juhudi kuona ya kwamba hali hiyo inakomeshwa.

Alisema tayari amezungumza na katibu katika wizara ya ardhi Bw Nicholas Muraguri ambaye alisema ifikapo Januari kila jambo katika afisi ya ardhi litaendeshwa kwa njia ya kidijitali.

“Nilifanya kikao na katibu huyo mnamo Ijumaa wiki jana katika afisi yake na tukakubaliana kuwa maafisa katika wizara hiyo watazuru Thika mwezi Januari na kuweka kliniki ya mwezi mzima ili kuhamasisha wananchi kuhusu maswala ya ardhi,” alisema Bw Wainaina.

Alisema mawakala wamekuwa kikwazo kikubwa katika ununuzi wa vipande vya ardhi katika eneo hilo.

Aliitaka serikali kuchukua hatua kuona ya kwamba inakomesha mara moja walaghai wa ardhi.

Kwa muda mrefu wakongwe wamekuwa wakilengwa na watu hao kwa kuwalaghai huku ardhi zao zikiuzwa kwa watu wasiojua.

“Imedaiwa pia maafisa wengine kwenye afisi za huduma za masuala ya ardhi wanashirikiana na walaghai hao ili kuwahadaa wananchi,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo jana Jumatatu, alipozuru afisi ya naibu kamishna wa Thika Magharibi, Bw Mbogo Mathioya aliyepata uhamisho hadi Thika wiki chache zilizopita.

Alisema afisi ya ardhi imepata malalamishi mengi kuhusu ulaghai unaoendeshwa kila mara na mawakala hao.

Kwa muda mrefu mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya unyakuzi wa ardhi mjini Thika.

Miezi miwili iliyopita alitetea unyakuzi wa ekari moja ya ardhi iliyonyakuliwa na ilikuwa imepangiwa na serikali kujenga maktaba ya umma.

Mwaka wa 2019 Wizara ya Ardhi ilituma maafisa wake kuchunguza malalamishi ya wakazi wa Ruiru, Kaunti ya Kiambu ambapo shughuli hiyo ilichukua muda wa miezi mitatu mfululizo.

Naibu kamishna Bw Mbogo Mathioya alisema tayari amepata malalamishi hayo na maafisa wa upelelezi wataanza kufanya uchunguzi ili kuwanasa wahusika.

“Inasikitisha kuona ya kwamba watu wengi wanapoteza vipande vyao vya ardhi mbele ya walaghai. Serikali haitakubali jambo kama hilo kuendelea,” alisema Bw Mathioya.

You can share this post!

Kenya kushiriki vipute vya Cecafa vya kufuzu kwa fainali za...

Serikali yasema Huduma Namba itaboresha maisha ya Wakenya