BBI yapendekeza Chebukati na wenzake wapigwe kalamu
Na CHARLES WASONGA
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu watapigwa kalamu kabla ya muhula wao kukamilika tume hiyo itakapoundwa upya.
Kulingana na ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) iliyozinduliwa Jumatano, mwenyekiti mpya na makamishna wengine sita watateuliwa chini ya mfumo mpya wa kisheria ambapo vyama vya kisiasa vitapendekeza watu watakaoteuliwa kwa nyadhifa hizo.
“Ili kuhakikisha kuwa IEBC inaendesha uchaguzi kwa njia huru, yenye haki na itakayoaminika, imependekezwa kwamba viongozi wa vyama vya kisiasa wahusishwe katika uteuzi wa makamishna. Aidha, hii itajenga imani ya vyama hivyo kwa IEBC kupitia uungwaji mkono kutoka kwa wagombeaji,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mjini Kisii.
Ili kuimarisha utendakazi wa sekritarieti ya IEBC na kuzima ufisadi ripoti hiyo inapendekeza kuwa wafanyakazi wote wa afisi hiyo kuu watahudumu kwa kandarasi ya miaka mitatu. Kandarasi hiyo inaweza kuongezwa mara moja pekee.
“Vile vile, hii itahakikisha kuwa makamishna wapya wa tume hiyo hawatakuwa mateka wa sekritariati hiyo na hivyo kuibua migongano na mivutano ya kila mara,” ripoti hiyo inaongeza.
Ili kuimarisha imani ya wagombeaji viti kwa Maafisa wa Kusimamia Uchaguzi (ROs) uajiriwa wao utafutwa chini ya mfumo utakaotumiwa kuwateua makamishna wa IEBC kulingana na ripoti hiyo.
Hii ina maana kuwa viongozi wa vyama vya kisiasa watahusishwa katika mchakato mzima wa uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi zote.
“Vile vile, wasimamizi wa uchaguzi watafanya kazi kama vibarua na hawataruhusiwa kusimamia zaidi ya uchaguzi mmoja,” inaeleza ripoti hiyo.
Mageuzi mengine ambayo yanapendekezwa kufanyiwa IEBC ni kwamba sio lazima mwenyekiti awe mwanasheria ilivyo katika sheria ya sasa.
Kulingana na ripoti, mtu ambaye atachaguliwa kwa wadhifa huo sharti awe na tajriba ya miaka 15 katika cheo cha usimamizi katika asasi yoyote inayotambulika, miongoni mwa mahitaji mengine.
“Vile vile, mwenyekiti wa IEBC pia ameongezewa mamlaka zaidi ambapo atahudumu kama afisa mkuu mtendaji wa asasi hiyo. Hii itapunguza migongano na mivutano kati ya washikilizi wa afisi hizo mbili,” ripoti hiyo inasema.