Habari Mseto

Matumaini ya BBI kuinusuru sekta ya kilimo

October 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KENNEDY KIMANTHI

RIPOTI ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) imetoa mapendekezo ya kuimarisha sekta ya kilimo na kuwazima wafanyabiashara walaghai ambao wamefyonza wakulima kwa miaka mingi.

BBI inapendekeza vita dhidi ya ufisadi kunusu sekta ya Kilimo na pia kupendekeza marekebisho ambayo yakitekelezwa, yatapiga jeki uchumi unaoendelea kuporomoka.

Pia, stakabadhi hiyo inapendekeza afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), iongezwe mamlaka ili ipambane na ufisadi kwenye sekta za kilimo na ufugaji. Inapendekeza kesi za ufisadi katika sekta hizi isikizwe na kuamuliwa haraka jinsi tu zile zinazohusu malalamishi baada ya uchaguzi mkuu.

“Upanuzi wa uwekezaji katika kilimo na ufugaji na kuelekeza juhudi katika kupambana na wafanyabiashara wakora ambao huwashika wakulima mateka. Watu wengi hutegemea kilimo na hakuna njia ya haraka ya kuwaondoa kwenye ufisadi,” ikasema ripoti hiyo.

Wadadisi na wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema, sekta ya kilimo imetelekezwa kwa miaka mingi na ndio sababu taifa hukabiliwa na ukosefu wa chakula tangu uhuru.

Vilio vya wakulima vimekuwa vikitanda kila mara nchini huku wakidai serikali imekosa kuweka juhudi za kutosha kuhakikisha wanapata mapato mazuri.

Mnamo Januari mwaka huu, malalamishi hayo yaligusa Rais Uhuru Kenyatta na akaamrisha mabadiliko ya kisera yatekelezwe na pesa zaidi ziwekezwe katika kilimo cha majani chai, kahawa, mpunga na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Kenya hupata mapato mazuri kutokana na mauzo ya kahawa, majani chai na maua.

Kwenye mabadiliko hayo, Mwangi Kiunjuri alifutwa kazi kama Waziri wa Kilimo na nafasi yake ikachukuliwa na Peter Munya.

Kati ya masuala ambayo yametajwa na Wakenya kama yanayoathiri sekta ya Kilimo ni ukosefu wa sheria kudhibiti ushindani, uwepo wa mashirika kadhaa ya serikali ambayo majukumu yao hugongana na mazingira magumu yanayowazima wawekezaji wa kibinafsi.

Ingawa ukosefu wa sheria na sera thabiti ni masuala ambayo yamekuwa yakilalamikiwa, huenda hakutakuwa na mabadiliko iwapo serikali haitatoa fedha za kutosha kufadhili sekta ya kilimo.

Ripoti ya BBI inaamrisha serikali itenge asilimia 10 ya bajeti yote kuimarisha sekta ya kilimo na kuimarishwa kwa mauzo ya mazao kupitia bei nzuri ya kuwaridhisha wakulima.

“Serikali itashirikiana na wadau kwenye sekta ya kibinafsi kuwashauri wakulima. Pia kilimo cha mimea na ufugaji kitapanuliwa huku wakulima wakihimizwa kutumia njia za kisasa kuhakikisha wananufaika kimapato,” ikaongeza ripoti ya BBI.

Inahimiza ujenzi wa viwanda vya kutengeneza bidhaa na pia ya kutayarisha vifaa vya kilimo. Pia inapendekeza teknolojia itumike kuongeza uzalishaji.

BBI pia inapendekeza kuongezwa nguvu kwa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji (KALRO), Mamlaka ya Uvuvi na Chakula (AFFA) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (KARI) kama njia ya kuimarisha juhudi za utafiti na uvumbuzi.

Wakati wa kutoa maoni, wadau mbalimbali walikuwa wamezua maswali kuhusu ukosefu wa ufadhili kwa sekta ya kilimo kutoka kwa serikali kuu na ile ya kaunti.