• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
ODM yatafuta fimbo ya kumnyamazisha Jumwa kwenye ugavana 2022

ODM yatafuta fimbo ya kumnyamazisha Jumwa kwenye ugavana 2022

Na ALEX AMANI

CHAMA cha ODM kimo mbioni kumtafuta mgombea atakayemenyana na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kaunti ya Kilifi mwaka wa 2022, huku chama hicho kikisemekana kuwa na wakati mgumu kupata mwaniaji mashuhuri zaidi.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa katika kaunti hiyo Alfred Katana, kwamba chama cha ODM kimejaribu kuwapima uzito wagombea kadhaa, akiwemo mbunge wa Magarini Micheal Kingi ambaye ni kakake mdogo gavana wa kaunti hiyo Amason Kingi ili kuangalia iwapo ana uwezo wa kukabana koo na Jumwa.

“Kufikia sasa hapa Kilifi chama cha ODM bado hakijapata mgombea anayeweza kukabana koo na Aisha Jumwa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha ugavana ifikapo 2022. Kwa sababu ukiangalia hata majina yaliyoko kwenye orodha ya wagombea na chama cha ODM bado wengi wao hawana uwezo wa kuishawishi jamii ya Kilifi kuwapigia kura na wengine hawawezi hata kujitetea au hata kujieleza mbele ya jamii,” alisema Bw Katana.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kilimgeukia aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro ili kuangalia uwezo wake iwapo anaweza kumpiku Jumwa kwenye kinyang’anyiro hicho,

Lakini bado hakikutosheka na uwezo wake kutokana na kukosa kwake kumakinika katika kuhutubia umma kwenye majukwaa ya kisiasa, mikutano ya hadhara jambo ambalo limekifanya chama hicho kutilia shaka ushawishi wake kwa wapiga kura.

Hatua iliyokilazimu chama cha ODM kurudi tena mezani na kujadili upya jambo hilo ambapo jina lingine lililoibuliwa na kuwekwa kwenye orodha hiyo ya wagombea wanaopigiwa upatu na chama hicho kumrithi Gavana Kingi lilikuwa la afisa wa serikali ya kaunti hiyo Kenneth Kazungu almaarufu Tungule.

Chama kilimchanganua kwa kina na kusema bado hana uwezo wa kubwaga Jumwa kwenye kinyang’anyiro hasa ikizingatiwa kwamba Kazungu anajulikana kuwa anapigania ubunge wa Ganze na isitoshe ana uhusiano mzuri na Jumwa na itakuwa vigumu kumpinga.

Hata hivyo, chama cha ODM kwa sasa kinadaiwa kuelekeza macho yake kwa Seneta wa kaunti hiyo Steward Madzayo kuangalia uwezo wake iwapo anaweza kukabana koo na Jumwa, jambo ambalo limekiacha chama hicho kimesalia katika njia panda ya kufanya uamuzi wa ni nani atakayepeperusha bendera ya chama hicho ifikapo 2022. Hali hiyo imechochewa na umaarufu wa Mbunge huyo wa Malindi ambao unazidi kukua kila uchao katika kaunti hiyo.

Inaaminika kwamba ODM sasa inategemea kesi zinazomkabili Aisha Jumwa mahakamani iwapo atapatikana na hatia kama kigezo pekee ili kumzuia kugombea kiti cha ugavana huku chama hicho kikidaiwa kuomba usiku na mchana mbunge huyo apatikane na hatia ili afungiwe nje.

ya uchaguzi kwa sababu kinahofia kwamba wagombea wake hakuna hata mmoja anayeweza kumubwaga Jumwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Hatua hii imekifanya chama hicho kinapata wakati mgumu wa kufanya maamuzi wa ni nani atakayepeperusha bendera ya chama hicho hapa Kilifi ifikapo 2022 maana kinahofia kisipokuwa makini huenda kikaibishwa na mbunge huyo. Ndio maana chama hicho kimekuwa kikiomba usiku na mchana mbunge huyo apatikane na hatia ili afungiwe nje kwenye uchaguzi huo asipate kushiriki kwani wahisi atawashinda iwapo atashiriki.” aliongeza Bw Katana.

Lakini juhudi za chama hicho huenda zikakosa kuzaa matunda kwenye kesi ya mauaji inayomkabili mbunge huyo mahakamani kufuatia uwepo wa siasa ndani yake.

Kinachozidi kukanganya chama hicho ni kimya cha gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi ambaye inasemekana anaunga mkono vuguvugu la muungano wa wapwani kwa jumla unaosimamiwa na mbunge huyo wa Malindi.

Mbali na hayo ODM inaaminika kupoteza wengi wa wanasiasa maarufu katika ukanda wa Pwani kufuatia wasiasa hao kuunga mkono vugu vugu la umoja wa wapwani ili kuunda chama chao kitakacho wawakilisha kwenye uchaguzi mkuu ujao wakiamua kuachana kumuunga mkono Raila Odinga katika ukanda huo wa Pwani.

You can share this post!

Magufuli aahidi uchaguzi huru kampeni zikitamatika leo

AFYA: Miaka 17 baadaye bado chozi linamtiririka…