BBI: IEBC kupata makamishna wapya kabla ya refarenda
Na CHARLES WASONGA
MAANDALIZI ya kura ya maamuzi kuhusu mageuzi ya Katiba yaliyopendekezwa katika ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) yamepigwa jeki baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada wa kufanikisha uteuzi wa makamishna wapya wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Jana, Rais Kenyatta alitia saini mswada wa marekebisho ya sheria ya tume hiyo inayopendekeza kuundwa kwa jopo litakaloteua makamishna kujaza nafasi ya wanne waliojiuzulu.
Waliojiuzulu ni Dkt Roselyn Akombe mnamo Oktoba, 2017 pamoja na Bi Connie Nkatha, Margaret Mwachanya Wanjala na Dkt Paul Kurgat waliojiondoa mnamo Aprili 18, 2021.
Baada ya kujiondoa kwa wanne hao, IEBC imekuwa ikiendesha na mwenyekiti Wafula Chebukati pamoja na makamishna wawili; Abdi Guliye na Boya Molu.
Tume hiyo haiwezi kufanya maamuzi muhimu ya kisera na kifedha ikiwa na makamishna watatu kwani, kisheria, maamuzi hayo yanapasa kupitishwa na angalau makamishna watatu.
Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya alidokeza kuwa kutiwa saini kwa mswada huo utaipa IEBC uwezo wa kuendesha kura ya maamuzi kuhusu mageuzi ya Katiba ifikapo Juni, 2021.
“Kutiwa saini kwa mswada huu sasa kutatoa nafasi kwa makamishna wapya sasa kuteuliwa haraka kujaza nafasi ya wanne walioondoka ili kuiweka IEBC tayari kwa kuandaa kura ya maamuzi kabla ya Juni mwaka ujao,” akasema.
Kuidhinishwa kwa sheria hiyo kunaonekana kwenda kinyume na matakwa ya wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto waliotaka jopo hilo la uteuzi kuwa na wanachama 11.
Hata hivyo, majuzi Dkt Ruto alifafanua kuwa suala muhimu kwake sio atakayeongoza IEBC kwani mshindi katika uchaguzi mkuu ujao ataamuliwa na wapiga kura.
“Hatuna shida na yule ataongoza IEBC. Tunachofahamu ni kwamba mshindi katika uchaguzi wa urais ataamuliwa na wapiga kura. Wanaweza hata kumteua Oburu Odinga (Kakake Raila) kuwa mwenyekiti wa IEBC. Sijali. Kile ninachojua ni kwamba hawataweza kuamua. Ni wananchi wataamua,” akasema alipohudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Total Grace, mjini Embu mnamo Oktoba 11.
“Kile ningependa kuwaambia washindani wetu ni kwamba: Mwaweza kuteua makamishna mnaowataka. Mwaweza kuwa na mwenyekiti wa IEBC mnayemtaka. Lakini tafadhali mtupe hakikisho kwamba wananchi watakapoamua tafadhali mkubali matokeo na msisababishe fujo,” Dkt Ruto akaongeza baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Total Grace mjini Embu.
Kwingineko, Mkurugenzi wa masuala ya elimu kwa wapigakura katika IEBC Immaculate Kassait jana alikuwa na wakati mgumu kujiondolea lawama aliyoelekezewa na upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hii ni kuhusiana na utata uliogubika matokeo ya kura ya urais ambapo alikuwa miongoni mwa maafisa wa tume hiyo waliolaumiwa kuficha data muhimu za hesabu za kura.
Bi Kassait ambaye aliteuliwa na Rais Kenyatta kuwa Kamishna wa Data alikuwa akipigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Mawasiliano kubaini ufaafu wake kwa cheo hicho.
Bi Kassait alijitenga na lawama za wizi wa kura akisema wakati huo alikuwa mkurugenzi wa usajili wa wapiga kura na hakuhusika na masuala ya matokea ya uchaguzi.“Hata hivyo, ningependa kuihakikishia kamati hii kuwa maajenti wa vyama vyote vya kisiasa walifunguliwa sava,” akasema.