NGILA: Huduma Namba itumie ‘Blockchain’ kufanikiwa
NA FAUSTINE NGILA
Jina langu kwenye kitambulisho ni Faustine, lakini ajenti wa M-Pesa aliyenisajili kwenye huduma hiyo ya kutuma na kupokea pesa alikosea herufi ya kwanza la jina langu na kunisajili kama Eustine.
Licha ya juhudi zangu za kujaribu kurekebisha tegu hilo kwenye jina langu, limesalia vile vile kila ninapotumia huduma hiyo. Hii inamaanisha ukishasajiliwa kwenye mtandao huo, ni vigumu kubadilisha, na kosa hilo litasalia milele.
Hapo ndipo kuna tatizo kuu. Iwapo mtu atasajiliwa kwa jina lisilofanana herufi kwa herufi na lile lililo kwa kitambulisho chake, basi mtu huyo anaweza kukwepa vipengee kadhaa vya kisheria na kuwatesa wenzake kimakusudi.
Tuseme, kwa mfano, ametumiwa Sh250,000 kwa M-Pesa kimakosa kisha akatae kumrudidishia aliyetuma, je, aliyetuma atamshtaki nani? Aliyepokea atakuwa na ujasiri wa kusema si yeye alitumiwa hela hizo kwa kuwa jina lake la M-Pesa halifanani na lile la kitambulisho, na hivyo korti itatupa kesi hiyo.
Hii ndiyo taswira kamili ya changamoto za utambulisho wa kijumla hapa barani Afrika. Utampata raia wa Burundi humu nchini amejisali kwa huduma za maongezi, M-Pesa na hata benki akitumia kitambulisho cha Mkenya.
Ni dhahiri kuwa maelfu ya wanafunzi wamejisajili kwenye huduma hizi wakitumia vitambulisho vya wazazi wao na hata babu zao.
Juzi nilipigwa na butwaa kuona ujumbe mmoja pale Twitter mtumizi mmoja akijipiga kifua jinsi Safaricom hawawezi kumnasa kirahisi kwa maovu anayofanya kwa kuwa alijisali akitumia kitambulisho cha nyanya yake aliyefariki zamani!
Kutokana na hili, serikali ya Kenya hivi majuzi imekuwa mbioni kuvumisha mradi wa Huduma Namba, Wakenya 12 tayari wakimiliki kadi zao.
Ingawa ni hatua nzuri inayolenga kuondoa kasoro katika utambulisho wa wananchi kidijitali, sina imani na jinsi mradi huo unaendeshwa. Huenda usitoe suluhu za maana kwa visiki hivi.
Ikiwa serikali inanuia kumaliza uhuni wa mitandaoni na kusawazisha data ya wananchi wote, basi mbona isitumie mfumo wa teknolojia ya blockchain? Kinachohitajika tu ni kukusanya data yote ya Wakenya kwenye seva za serikali na kuipakia kwa mfumo wa kidijitali, kisha kuwasajili kwenye mfumo huo kwa kutumia majina yao halisi na nambari za vitambulisho.
Data yote kuhusu kila mtu kama nambari ya simu, nambari ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), nambari ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), nambari ya Hazina ya Bima ya Afya nchini (NHIF), picha ya uso, aina ya damu, alama za vidole, historia ya elimu, cheti cha kuzaliwa, cheti cha ndoa, nambari za kaunti za benki, mashirika na hata vitambulisho vya kitaaluma yafaa kuunganishwa kwenye mfumo huo.
Mtu anapofariki basi data katika mtandao huo yafaa kuonyesha hayupo tena na taarifa zake haziwezi kutumika tena.
Hii ndiyo suluhu tosha kuzima wizi wa mitandaoni, uuzaji wa bidhaa ghushi na ulanguzi wa binadamu.
Ninaishangaa serikali kwa kuwa licha ya kuunda Jopokazi la Blockchain linaloshughulikia matumizi ya teknolojia hii humu nchini, haina nia ya kutumia mapendekezo yaliyotolewa kuhusu kuondoa vizingiti vya utambulisho wa wananchi.
Kwa kutekeleza mradi wa Huduma Namba tukitumia blockchain, basi matatizo mengi ya utambulisho ambayo tumeshuhudia kortini na hata kwenye uchaguzi yatatoweka yenyewe.
Lakini iwapo serikali itatekeleza mradi huo bila teknolojia hii, basi ni hadaa tupu kwamba inalenga kuwasaidia Wakenya, ni kisa tu kingine cha matumizi mabaya ya ushuru tunaolipa kila siku.