• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Pigo kwa Bunge huku mahakama ikizima sheria 23

Pigo kwa Bunge huku mahakama ikizima sheria 23

Na JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA Kuu imebatilisha Sheria 23 zilizopitishwa na Bunge la Taifa bila mchango wa seneti, ikisema zimekiuka Katiba.

Majaji watatu wa Mahakama Kuu waliamua kuwa, mchango wa seneti katika kupitishwa kwa sheria hizo hauwezi kupuuzwa na kwamba, bunge ilikiuka katiba kutoishirikisha.

Majaji hao Jairus Ngaah, Anthony Ndung’u na Teresiah Matheka walibatilisha sheria hizo kwa kuwa seneti haikutoa msimamo wake.

Walisema kwamba sheria yoyote inayohusu serikali za kaunti na ugatuzi haziwezi kupitishwa bila mchango wa seneti.

Katika uamuzi wao, majaji hao walisema spika mmoja wa mabunge yote mawili hawezi kufanya uamuzi unaohusu serikali za kaunti peke yake bila kushauriana na mwenzake.

“Ni lazima na hitaji la kikatiba kwamba, mswada wowote unaochapishwa na moja ya mabunge hayo uwasilishwe kwa lingine liamue uwe ni mswada spesheli au wa kawaida. Uamuzi huo unategemea kukiwa na utata kuhusu iwapo kaunti zitahusika,” majaji walisema.

Hata hivyo, majaji hao waliamua sheria hizo ziendelee kutumika kwa miezi tisa ili kutoa muda kwa mabunge hayo mawili kurekebisha mambo.

Walisema kwamba, ndani ya muda huo, Bunge la Kitaifa linafaa kutekeleza hitaji la kikatiba na kuwasilisha sheria hizo kwa seneti.

Likikosa kufanya hivyo, sheria hizo zitakuwa zimefutwa baada ya miezi tisa. Sehemu ya tatu ya kifungu nambari 110 cha katiba inasema kwamba, maspika wa mabunge yote mawili wanafaa kushirikiana kutatua mzozo ukizuka kuhusu iwapo mswada unagusia masuala ya kaunti uwe mswada spesheli au wa kawaida.

Sehemu ya nne ya kifungu hicho inasema kwamba, mswada wowote unaohusu serikali za kaunti ukipitishwa na bunge moja, spika wa bunge hilo anapaswa kuuwasilisha kwa spika wa bunge lingine.

Seneti iliwasilisha kesi hiyo mwaka jana baada ya bunge la taifa kupitisha sheria hizo 24 ikilalamika kuwa haikuhusishwa.

Maseneta walilalama kuwa, wabunge walikuwa wakiwapuuza katika utungaji wa sheria, jambo ambalo ni kinyume cha katiba. Moja ya sheria zinazoathiriwa na uamuzi huo ni ile ya Afya ya Taifa ambayo ilifanyia mabadiliko masuala ya afya.

Ingawa afya ni jukumu lililogatuliwa, bunge la taifa lilipitisha sheria hiyo bila kuhusisha seneti.

Sheria hiyo ilipatia Mamlaka ya kusambaza dawa na vifaa vya matibabu (KEMSA) kibali cha kuuzia serikali za kaunti dawa na vifaa vya matibabu.

Kufuatia sheria hiyo, serikali za kaunti hazifai kununua dawa na vifaa kutoka kwa shirika na kampuni nyingine.

Sheria nyingine muhimu iliyoathiriwa na uamuzi huo ni iliyozua utata ya uhalifu wa kutumia mtandao na kompyuta ambayo ililenga wanablogu na wanaotumia intaneti.

Kulingana na sheria hiyo, mtu anaweza kufungwa jela miaka kumi au kutozwa faini ya Sh20 milioni au adhabu zote mbili kwa kunyanyasa mwingine kwa kuchapisha habari kumhusu zinazoudhi kwenye mtandao.

Sheria hiyo inatoa adhabu sawa kwa wanaoandika habari zinazoweza kufanya mtu kuingiwa na hofu ya kuzuka kwa ghasia, uharibifu au kupotea kwa mali yake.

You can share this post!

Magavana waliovuta ?mkia sasa wajitetea

Wamuua kaka yao wakipigania mahari ya dada