• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Ruto aitetea IEBC

Ruto aitetea IEBC

MWANGI MUIRURI na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto amemtetea vikali mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, dhidi ya lawama kutoka kwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.Bw Odinga amekuwa akishinikiza tume hiyo kufanyiwa mageuzi, akiitaja kuwa chanzo kikuu cha matatizo ambayo huikumba nchi baada ya kila miaka mitano.

Bw Odinga pia ameikosoa vikali tume, baada ya kusema itaigharimu Kenya Sh14 bilioni kuandaa kura ya maamuzi kupitisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Kiongozi huyo amekuwa akisisitiza zoezi hilo halipaswi kuigharimu nchi zaidi ya Sh2 bilioni.Lakini jana, Dkt Ruto alimtetea vikali Bw Chebukati, akisema machungu ya Bw Odinga dhidi ya tume yanatokana na hatua ya kutomtangaza mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais katika chaguzi kuu zilizopita.

“Kuna watu wana hasira kuhusu IEBC, tume hiyo huwa haipigi kura. Wananchi ndio huwa wanafanya maamuzi kwenye chaguzi. Ikiwa wananchi wamefanya maamuzi yao, mbona unaelekeza hasira zako kwa tume? Ndipo mnasikia (Raila) akipiga kelele kwani bado ana shida nayo. Amekuwa na tatizo hilo tangu zamani. Amevunja tume tatu kufikia sasa. Alivunja tume zilizoongozwa na mabwana Samuel (Kivuitu), Isaac (Hassan) na sasa Bw Chebukati,” akasema.

“Sababu kuu ya hasira yake ni kwamba anataka uwepo wa tume ambayo itamtangaza kuwa Rais, hata ikiwa hana kura za kutosha. Hilo linawezekana?” akashangaa Dkt Ruto.

Alisema inashangaza kuwa mnamo 2010, wakati Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu, tume ilitumia Sh10 bilioni kuandaa zoezi hilo, ambapo nchi ilikuwa na wapigakura 12 milioni waliosajiliwa.

“Inawezekana vipi kutugharimu Sh2 bilioni kuandaa kura ya maamuzi kwa wapigakura 20 milioni wakati ilitugharimu Sh10 bilioni kwa zoezi kama hilo kwa wapigakura 12 milioni?” akauliza. Hata hivyo, chama cha ODM jana kilimtetea vikali Bw Odinga, kikisema lengo la IEBC na maafisa wake wakuu ni kuipora nchi kupitia sakata ya ufisadi kama ya Chickengate.

Kwenye sakata hiyo, baadhi maafisa wakuu wa zamani wa tume walishtakiwa kwa tuhuma za kupokea hongo kutoka kwa kampuni ya Smith and Ozman kutoka Uingereza ili kuipa kandarasi ya kuchapisha karatasi za uchaguzi mkuu.

“Lengo kuu la Bw Chebukati na maafisa wake katika tume ni kuendeleza kutowajibika kwao, ambapo Bw Odinga ndiye amekuwa mwathiriwa mkuu kwa muda mrefu,” akasema Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.Alisema kuwa mchakato wa BBI unalenga kuifanyia tume hiyo mabadiliko kamili.

“Ikiwa kuna wakati mwafaka wa kuifanyia mabadiliko tume, basi ni sasa. Hatuwezi kuendelea kushuhudia matokeo ya kutowajibika kwake,” akasema.

Ripoti ya BBI inapendekeza mageuzi kadhaa kwenye tume hiyo, baadhi yakiwa uteuzi wa makamishna wapya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta alitia saini mswada unaopendekeza kuajiriwa kwa makamishna wanne wapya katika tume, baada makamishna waliohudumu awali kujiuzulu kutoka nyadhifa zao.

You can share this post!

MUTUA: Iwe ni Trump au Biden, watakusaidia nini vile?

Injera na wenzake kupimwa tena corona kabla ya kushiriki...