• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Wakulima wataka NCPB ipewe fedha

Wakulima wataka NCPB ipewe fedha

STANLEY KIMUGE na WYCLIFF KIPSANG

WAKULIMA wa mahindi eneo la Bonde la Ufa wametoa wito kwa serikali kuharakisha kutoa pesa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) ili kuiwezesha kununua mahindi kutoka kwao.

Wakulima hao wamekuwa wakichelea kupeleka mazao yao katika maghala ya NCPB kwa sababu bodi hiyo haina hela za kuwalipa.Walitoa wito kwa serikali kuharakisha utekelezaji wa kanuni kuhusu mfumo wa Upokezi wa Mabohari ili kuhakikisha wakulima wananufaika kutokana na zao hilo.

“Kwa sasa, hatujui iwapo NCPB inafanya kazi kwa kutumia mfumo wa zamani au mpya. Kanuni hizo zinapaswa kupitishwa katika mchakato wa kushirikisha umma na wakulima kabla ya kuchapishwa rasmi,” alisema Mkurugenzi wa Muungano wa Wakulima Nchini (KFA) Kipkorir arap Menjo.

Aidha, wametoa wito kwa serikali kuu na za kaunti kusaidia vyama vya mashirika kupata mitambo ya kukaushia nafaka inayoweza kwenda maeneo mbalimbali ili kuwawezesha kudhibiti hasara msimu huu kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Wakulima hao wamekuwa wakichelea kupeleka mazao yao kwa NCPB kutokana na bei za chini zinazotolewa na serikali.Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika maeneo mbalimbali unaonyesha kuwa baadhi ya wakulima wameanza kuvuna mazao yao.

Zao hilo linauzwa kati ya Sh1, 700 na Sh2, 300 kwa kila gunia ya kilo 90.Bw Elijah Bett, mkulima wa mahindi kutoka eneo la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu, alisema serikali ni sharti inunue mahindi kwa Sh3,000 kwa kila gunia la kilo 90 ili kuwawezesha kupata faida kutokana na gharama kuu ya uzalishaji.

Rais Uhuru Kenyatta aliamuru Wizara ya Kilimo mwezi uliopita kuhakikisha kuwa wakulima wanauza mahindi yao kwa bei ya zaidi ya Sh2, 500.

Hata hivyo, Bw Bett alisema gharama ya uzalishaji ilipanda mno kwa sababu walilazimika kununua mbolea na vifaa vingine vya kilimo kwa bei ghali wakati serikali ilipositisha mradi wa kupunguza bei ya mbolea msimu uliopita.

“Haina maana kwetu kupeleka nafaka kwenye mabohari kutokana na gharama ya juu ya uzalishaji. Wakulima wanahitaji kulipwa bei nzuri kwa sababu tunahitaji kulipa karo, kulipa mikopo na pia kujitayarisha kulima mashamba yetu,” alieleza Bw Bett.

Aidha, alisema kwamba msimu huu wanatarajia mavuno tele ya mifuko 30 kwa kila ekari ikilinganishwa na mifuko 15 msimu uliopita kutokana na hali njema ya anga mwaka huu.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Vijana wawe makini kabla ya kufanya uamuzi...

Ole Lenku aidhinishwa kuwa msemaji wa jamii ya Wamaasai