Mgavana watofautiana kuhusu sheria ya kuwataka madiwani kuwa na digrii
Na ERIC MATARA
BAADHI ya magavana wametofautiana na wenzao kuhusu sheria inayohitaji wawaniaji wa viti vya udiwani kuwa na shahada ya digrii sawa na wawaniaji wa ubunge, wakiitaja kama isiyozingatia haki.
Magavana wanne waliozungumza pembezoni mwa mkutano wao mjini Naivasha, jana walipendekeza kuwa wawaniaji wa nyadhifa za udiwani wawe angalau na shahada ya diploma.
Hao ni pamoja na Ndiritu Muriithi (Laikipia), Kiraitu Murungi (Meru), Wycliffe Wangamati (Bungoma na Ali Roba (Mandera).“Kiwango cha juu zaidi cha kuhitimu kwa madiwani kinafaa kuwa shahada diploma. Hiyo itakuwa imetosha,” akasema Gavana Murungi.Kauli yake iliungwa mkono na Bw Wangamati akisema:
“Si haki kuwekea madiwani kiwango zaidi ya hapo; digrii ni juu zaidi.” Magavana hao walisema hatua ya kupandisha kiwango cha masomo cha madiwani itawafungia nje watu wengine ambao wangetaka kuwania.
Hata hivyo, Gavana Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na mwenzake wa Siaya, Bw Cornel Rasanga, walitofautiana na kauli za wenzao wakisema madiwani wanapaswa kuwa na elimu ya kiwango cha digrii.
“Hata wapishi wanafaa kuhitimu kiwango fulani. Hawa ni watu ambao watakuwa wakishiriki katika uundaji wa sheria na kufuatilia utendakazi wa magavana na maafisa wao.
“Wanahitaji kuwa na masomo ya juu ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” akasisitiza Profesa Nyong’o.
Tayari madiwani wameapa kupinga sheria hiyo itakayohitaji wawaniaji wa viti vyao kuwa wamehitimu kwa digrii ya kwanza; na wametisha kwenda kortini kuibatilisha.
Kupitia Muungano wa Madiwani nchini (CAF) walisema sharti hilo litawafungia nje watu wengi ambao wangependa kuhudumu katika nyadhifa hizo za uongozi.
“Tutaenda kortini. Si haki kufungia nje watu wengine kwa misingi ya elimu ilhali kuna wananchi wako tayari kuwachagua,” alihoji mwenyekiti wa CAF, Bw Wahome Ndegwa, ambaye ni Spika wa Nyandarua.Alisema hitaji hilo, ambalo liko katika Sheria ya Uchaguzi 2012, linaweza kubagua viongozi wasio na digrii lakini wanazo sifa za kuwawezesha kutumikia wananchi.
“Hii sheria inakwenda kinyume na uhuru wa wananchi ambao, kikatiba, ni wao wenye uwezo wa kuamua nani anayefaa kuwaongoza,” Bw Ndegwa alieleza.Ingawa wengi wa madiwani wanakubali kwamba wanaotaka kuwania nyadhifa hizo sharti wawe wamesoma, wametaja hitaji la digrii “kuwa juu zaidi”.
Sheria hiyo, ambayo utekelezaji wake umeahirishwa mara kadhaa, inatazamiwa kuanza kutekelezwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.Mnamo 2017 wabunge walifanyia marekebisho sehemu ya 22 ya Sheria ya Uchaguzi, ambayo inaeleza kiwango cha elimu ya wanachama wa mabunge ya kaunti, Bunge la Kitaifa na Seneti.
Marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kuwa, wanaopania kuwania ubunge na udiwani sharti wawe na angalau shahada ya kwanza ya digrii kabla kupata idhini ya kuwania.
Ingawa kanuni hiyo ilipitishwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, wabunge walifanikiwa kuzima utekelezaji wake katika uchaguzi huo, kwa matarajio kwamba wale wasio na digrii watakuwa wamepata shahada hizo kufikia 2022. Kwa sasa ni wawaniaji wa kiti cha Rais, Naibu Rais, Gavana na Naibu Gavana pekee wanahitaji kuwa na digrii.