• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
BBI: Raila azima sherehe ya Ruto

BBI: Raila azima sherehe ya Ruto

VALENTINE OBARA na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM, Bw Raila Odinga, amepuuzilia mbali viongozi waliokuwa na matumani kwamba, ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ingefanyiwa marekebisho kabla kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.

Mnamo Jumatatu, Naibu Rais William Ruto na wafuasi wake ambao wanataka ripoti hiyo ifanywe marekebisho walieleza furaha yao kwamba, hatimaye kuna mikutano ya wadau itakayopelekea BBI kufanyiwa marekebisho.

Dkt Ruto alikuwa amepongeza hatua ya Bw Odinga kukutana na viongozi wa jamii ya wafugaji na kukubali mapendekezo yao wanayotaka yajumuishwe katika BBI.

‘Kujitolea kwa umma kurekebisha BBI ili ijumuishe mapendekezo haya ni hatua nzuri itakayozaa makubaliano. Mapendekezo haya pamoja na mengine yakikubaliwa, kuna nuru kuhusu mdahalo usiokuwa wa makabiliano,’ akasema Dkt Ruto, kwa maneno yaliyoashiria mwenye furaha na matumaini.

Naibu Rais na wandani wake hukosoa ripoti hiyo kuhusu masuala mbalimbali, hasa sehemu inayopendekeza upanuzi wa Afisi ya Rais ili kuwe na Waziri Mkuu na manaibu wake.

Kwa mtazamo wao, pendekezo hilo haliwezi kutatua changamoto kuhusu siasa za mgawanyiko ambalo ni miongoni mwa masuala yanayolengwa kutatuliwa na Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kupitia kwa BBI.

Jana, Bw Odinga alisema mikutano ya kujadili BBI inayoendelezwa kwa sasa ni kwa madhumuni ya kuhariri sehemu chache bila kubadilisha yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Alipokutana na Balozi wa China nchini Zhou Pingjian katika afisi yake iliyo Capitol Hill jijini Nairobi, waziri mkuu huyo wa zamani alisema kuna sehemu ambazo hazijaeleweka vyema ndio maana makundi mbalimbali yanapewa nafasi kupata ufafanuzi.

‘Ripoti hiyo ilivyo sasa imekamilika na hakuna uwezekano mkubwa kwamba mawazo mapya yatajumuishwa. Kuna makundi ambayo yanahisi maoni yao hayakujumuishwa jinsi walivyokuwa wamewasilisha wakati maoni yalipokusanywa, ndiposa tunaahidi kufanya uhariri,’ akaeleza Bw Odinga, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wake, Bw Dennis Onyango.

Kando na kikundi cha Tangatanga, makundi mengine ambayo yamelalamika kuhusu ripoti hiyo ni baadhi ya wakulima na magavana.Jana, Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa wametarajiwa kukutana na magavana kujadili BBI katika Kaunti ya Nakuru lakini hawakuwepo mkutanoni.

Baadhi ya mapendekezo ambayo magavana wanataka yajumuishwe katika BBI ni kwamba, kukiwa na ufujaji wa pesa na mali ya umma katika kaunti zao, wasishtakiwe kama hawajahusishwa moja kwa moja.

Magavana pia wanataka Seneti ipewe nguvu za kupitisha miswada bila kupitia kwa Bunge la Taifa, kuwe na nafasi ya Naibu Waziri atakayechaguliwa bungeni, pesa zote za mashirika ya serikali yanayotoa huduma zilizohamishwa kwa kaunti zikabidhiwe serikali za kaunti, na kaunti ziruhusiwe kuchukua mikopo ya fedha.

Vile vile, wanataka majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yafanyiwe ugatuzi, mgombea mwenza wa ugavana awe wa jinsia yoyote tofauti na pendekezo la BBI, kaunti zihusishwe kwenye masuala ya usalama, na viongozi wote wakuu wa kaunti walipwe pensheni wanapoondoka mamlakani.

Rais Kenyatta amekuwa akiepuka mzozano kuhusu ripoti ya BBI.Jana aliendelea kusisitiza kuwa tofauti za kisiasa zinaweza kutatuliwa kupitia kwa mazungumzo.

“Tuache siasa na tufanye kazi. Huu sio wakati wa kufanya siasa. Hakuna shida ambayo haiwezi kusuluhishwa tukiketi na kuwa na mjadala mwafaka,” akasema Rais.

Alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha mizigo cha shirika la reli jijini Nairobi.Kituo hicho kitawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo wanaoagiza bidhaa kutoka ughaibuni kuchukulia mizigo yao jijini Nairobi badala ya kusafiri hadi Mombasa.

Rais Kenyatta alionya wanasiasa dhidi ya kuchochea wafanyabiashara ambao soko lao litahamishwa ili kupisha ujenzi wa barabara ya kuelekea kituoni hapo kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari.

You can share this post!

Kesi za ufisadi za Sh224 bilioni zimekwama kortini –...

Sonko, Badi warushiana tope kuhusu taka mitaani