• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wito Waislamu wajihadhari na hafla za mazishi

Wito Waislamu wajihadhari na hafla za mazishi

Na LEONARD ONYANGO

BARAZA Kuu la Waislamu nchini (Supkem), limewataka Waislamu nchini kuendelea kujihadhari wakati wa kuandaa miili ya waathiriwa wa virusi vya corona licha ya wizara ya Afya kusema kuwa maiti haiwezi kueneza virusi.

Baraza la Supkem jana lilishutumu wizara ya Afya kwa kukosa kutoa mwongozo mpya kuhusu jinsi ya kuandaa maiti tangu iliporuhusu familia kuzika wapendwa wao waliofariki kwa corona miezi mitatu iliyopita.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Umma Francis Kuria mnamo Septemba, aliruhusu familia kuendesha mazishi ya wapendwa wao bila usimamizi wa maafisa wa afya huku akisema kuwa tafiti zimethibitisha kwamba maiti haienezi virusi vya corona.

“Ni kweli kwamba maiti haiwezi kueneza virusi vya corona kwa sababu haina uwezo wa kukohoa au kupiga chafya. Lakini ni vyema kutambua kwamba majimaji ya mwili yaliyoko kwenye ngozi yanaweza kusambaza virusi vya corona kwa watu wanaouosha,” akasema Prof Mohamed Karama, mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Waislamu ya kukabiliana na Virusi vya Corona (NMCRC).

Prof Karama alisema kuwa tangu serikali kuruhusu jamaa kuzika wapendwa wao, baadhi ya familia zimekuwa zikiosha maiti bila kuvalia mavazi ya kuwalinda dhidi ya virusi vya corona.

“Tangu serikali kutoa tangazo hilo, nyingi ya familia zimekuwa zikizika wapendwa wao bila kuhusisha vikosi maalumu vya Waislamu waliopewa mafunzo kuhusu jinsi ya kuendesha mazishi ya waathiriwa wa virusi vya corona.

“Tunashuku kuwa hali hiyo ndiyo imechangia katika ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo nchini,” akasema Prof Karama.

Vikosi maalumu vilivyopewa mafunzo ya kuzika waathiriwa wa corona kwa njia salama, vimeshiriki mazishi ya watu 250, haswa katika Kaunti ya Nairobi, Mombasa, Nakuru na Eldoret.

Kamati ya NMCRC imeagiza kuwa watu wanaoosha maiti (ghusl) kwa mujibu wa imani ya Kiislamu, wavalie mavazi ya kuwalinda dhidi ya virusi vya corona, maarufu PPE.

“Wakati wa kufanya ibada maalumu ya wafu (janaza) watu wazingatie masharti ya wizara ya Afya, ikiwemo kutokaribiana. Maji na eneo linalotumika kuoshea maiti linyunyiziwe dawa ya kuua virusi,” akasema.

Prof Karama pia aliwataka waombolezaji kutawanyika mara baada ya mazishi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Aliwataka Waislamu wanaohitaji msaada kuhusiana na mazishi ya waathiriwa wa virusi vya corona kuwasiliana na vikosi vya watu waliopewa mafunzo kupitia nambari ya simu: 0800 210 000.

Baraza la Supkem limewataka viongozi wa misikiti kote nchini kuhakikisha kuwa waumini wanavalia barakoa wakati wa sala na wanasimama umbali wa mita 1.5 kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na wizara ya Afya.

“Watu wanaoingia misikitini wapimwe joto na wapewe sabuni na maji safi ya kunawa mikono na misikiti pia inyunyiziwe dawa za kukabili corona mara kwa mara,” akasema mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado.

You can share this post!

Makanisa yatishia kupinga BBI

Utawala wa Donald Trump wajiandaa kwa awamu ya pili ya urais