Shujaa waalikwa kucheza Uhispania na Ufaransa kabla ya msimu ujao wa Raga ya Dunia
Na CHRIS ADUNGO
TIMU ya taifa ya wanaraga saba kila upande almaarufu Shujaa, imepata mwaliko wa kucheza nchini Uhispania na Ufaransa mnamo Februari 2021, mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kampeni za duru ya Raga ya Dunia.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Oduor Gangla amethibitisha kwamba wamepata mialiko hiyo kutoka Uhispania na Ufaransa na ameeleza matumaini kwamba vipute hivyo vitakuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Shujaa kwa muhula mpya.
“Mashindano ambayo tumealikwa kushiriki katika mataifa hayo yatapiga jeki maandalizi ya Shujaa kwa minajili ya Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande na michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan mnamo Julai 2021,” akasema Gangla.
Mbali na Kenya, vikosi vingine ambavyo vimealikwa kuchuana nchini Uhispania na Ufaransa ni New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa.
Kwa mujibu wa Gangla, washindani wa Shujaa katika vipute vya Raga ya Dunia na Olimpiki wamekuwa wakiendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mapambano mengine muhimu – jambo ambalo timu ya taifa inafaa pia kuanza kufanya.
“Hatuwezi kuendelea kukaa na kusubiri kwa sababu tuko nyuma ya ratiba. Washindani wetu wanafanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali katika mataifa yao,” akahoji Gangla.
Chini ya kocha mkuu, Innocent Simiyu, wanaraga wa Shujaa walifanyiwa vipimo vya corona wiki mbili zilizopita na wanatarajiwa sasa kuingia kambini kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.
Kwa mujibu wa Gangla, kampeni za msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya Cup zimeratibiwa kuanza rasmi mnamo Januari 16, hatua inayowapa vikosi muda wa kati ya wiki sita na nane kujiandaa.
Mnamo Novemba 12, 2020, KRU ilitaja kikosi cha wanaraga 29 ambao kwa sasa wataingia kambini kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 za kikosi cha Shujaa.
Mbali na ukaguzi wa kawaida utakaolenga kubaini hali zao za afya na uwezo wa miili kuhimili mazoezi makali, wanaraga wote hao walifanyiwa vipimo vya corona katika uwanja wa RFUEA, Nairobi kwa mujibu wa kanuni za mpya za serikali katika juhudi za kudhibiti msambao wa Covid-19.
Kati ya wanaraga ambao watategemewa na kocha Simiyu katika kampeni zijazo za Shujaa ni nahodha Andrew Amonde, kigogo Collins Injera anayeshikilia rekodi ya ufungaji wa idadi kubwa zaidi ya trai, Oscar Ouma, Willy Ambaka na Oscar Dennis.
Watano hao walikuwa sehemu ya kikosi cha SFX10 cha Afrika Kusini kilichonogesha kivumbi cha dunia cha wanaraga 10 kila upande cha IPL World 10’s nchini Bermuda majuzi.
Shirikisho la Raga Duniani (WR) tayari limefutilia mbali duru nne za kwanza za za Dubai, Cape Town, Sydney na Hamilton katika kampeni za Raga ya Dunia msimu ujao wa 2020-21.
Ina maana kwamba kipute cha Raga ya Dunia katika msimu wa 2020-21 kinaweza tu kung’oa nanga mnamo Machi 2021 kwa duru za Los Angeles (Amerika) na Vancouver (Canada).
Mbali na raga ya wachezaji saba kila kwa upande wa wanaume, Kenya itawakilishwa kwenye fani mbalimbali katika Olimpiki za Tokyo, Japan zikiwemo mbio za marathon, voliboli (wanawake), ndondi na taekwondo (wanawake na wanaume) na kupiga mbizi au uogeleaji (wanawake na wanaume).
“Nitategemea wanaraga waliopo kwa sasa katika orodha hii ya wachezaji wa Shujaa kabla ya kuwaweka kwenye mizani kwa mujibu wa viwango tunavyovihitaji. Tutaongeza orodha hiyo baadaye kwa kuleta wanaraga wapya kwa kuwa baadhi ya wachezaji tulionao kikosini wana mikataba inayoelekea kutamatika,” akasema Simiyu.
Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mwanzoni mwa Septemba 2020 kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni.
KIKOSI CHA SHUJAA:
Andrew Amonde, Vincent Onyala, Jacob Ojee, Geoffrey Okwach, Johnstone Olindi, Levy Amunga (KCB); Collins Injera, Billy Odhiambo, Daniel Taabu, Tony Omondi, Mike Okello (Mwamba); Sammy Oliech, Alvin Marube (Impala); Willy Ambaka, Herman Humwa, Eden Agero (Harlequins), Oscar Ouma, Nelson Oyoo (Homeboyz); Jeffrey Oluoch, Bush Mwale, Alvin Otieno (Nakuru); Harold Anduvate, Derrick Keyoga, Mark Kwemoi (Oilers); Daniel Sikuta, Brian Tanga (Kabras); Oscar Dennis, Dennis Ombachi (Nondescripts); Archadius Khwesa (Blak Blad).