• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Aliyetekeleza shambulizi Chuo cha Garissa ajinyonga selini

Aliyetekeleza shambulizi Chuo cha Garissa ajinyonga selini

Na MARY WAMBUI

RAIA wa Tanzania Rashid Charles Mberesero aliyehukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2019 baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki shambulizi la kigaidi mnamo 2015, alijitia kitanzi katika gereza la Kamiti, Ijumaa.

Msemaji wa idara ya magereza Kennedy Aluda jana Jumapili alieleza Taifa Leo kwamba, Bw Mberesero alipatikana amejitia kitanzi katika seli nambari 24 kwenye jumba la H.

“Alitumia blanketi kama kamba na kujinyonga. Mwili wake ulipatika ukining’inia kupitia dirishani ukiwa na blanketi shingoni,” akasema Bw Aluda.

Uchunguzi tayari umeanzishwa kubaini kilichomsukuma Bw Mberesero kujitoa uhai. Hata hivyo, marehemu alikuwa na tatizo la kiakili na alikuwa akipokezwa matibabu mara kwa mara.

Taarifa ndani ya gereza hilo zilisema marehemu alidungwa sindano Alhamisi kabla ya kujiua siku iliyofuata saa nane mchana.

Upasuaji wa maiti utafanywa kubaini chanzo kamili cha kifo chake.

“Uchunguzi huo hata hivyo lazima uhusishe familia yake iliyoko nchini Tanzania,” akaongeza Bw Aluda.

Bw Mberesero alikuwa akitumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia Chuo cha Garissa mnamo Aprili 2015. Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 150 ambao wengi walikuwa wanafunzi huku wengine 100 wakijeruhiwa.

Polisi walisema Jumapili walipokea ripoti katika kituo cha polisi cha Kahawa Magharibi kutoka kwa afisa anayehusika na masuala ya usalama katika gereza la Kamiti kwamba kuna mahabusu aliyekuwa amejitia kitanzi kwenye seli saa moja kasoro dakika 10 jioni.

“Maafisa wa polisi walitembelea seli hiyo nambari 24 kwenye jengo la H na wakapata mwili wa Rashid Charles Mberesero, raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 25 ukiwa umening’inia na umefungwa kwa blanketi shingoni na kwenye chuma cha dirisha,” ikasema ripoti kwenye kituo hicho cha polisi.

Marehemu alipatikana na hatia ya kupanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi na mahakama moja ya Nairobi. mwaka 2019.

Alihukumiwa maisha lakini wenzake Mohamed Abdi Abikar na Hassan Aden Hassan wakapewa hukumu nyingine. Rekodi za mawasiliano kwenye simu na maandishi yalithibitisha watatu hao walihusika na shambulizi hilo la kigaidi.

You can share this post!

Matumaini ya Sonko kujiokoa yamo kortini tu

COVID-19: Idadi jumla ya vifo nchini Kenya yafika 1,452