Kupungua kwa thamani ya shilingi kuwaongezea mzigo watumiaji stima Desemba
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA wataongezewa mzigo mkubwa wa bili za stima mwishoni mwa msimu wa sherehe za Krismasi kutokana na kodorora kwa thamani ya shilling ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni.
Kulingana na ratiba ya ada za umeme ya mwezi Desemba iliyochapishwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta Nchini (EPRA), ada zote za stima zitatozwa senti 69.77 kufidia ubadilishanaji wa sarafu za kigeni (Foreign Exchange Adjustment).
Mwezi jana wa Novemba bili za stima zilikuwa zikitozwa senti 55 kufidia mabadiliko ya sarafu.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa ongezeko kama hili kuwekwa katika bili ya stima kutokana na mabadiliko ya thamani ya sarafu za kigeni baada ya ongezeko la Sh1.07 lililoongezwa kwa kila kipimo cha stima mwezi wa Oktoba.
Mabadiliko katika ada ya mabadiliko ya thamani ya thamani ya sarafu yanayotekelezwa kila mwezi na mamlaka ya EPRA ni gharama inayotokana na ununuzi wa stima unaofanywa kwa kutumia sarafu za kigeni.
Kupungua mwa thamani ya sarafu ya Kenya kumesababishia Wakenya machungu kupitia kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma kutokana zinazoagizwa kutoka nje.
Kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 mwanzoni mwa mwaka huu, shilingi ya Kenya ilikuwa ya thamani ya juu, hali ambayo iliwanufaisha Wakenya kuwa kuwapunguzia gharama.
Kwa mfano katika miezi ya Februari na Machi, gharama ya mabadiliko ya sarafu ilipungua zaidi kiasi kwamba watumiaji stima walikuwa wakirejeshewa bakshishi. Hii ni kutokana na sababu kwamba thamani ya shilingi ilikuwa imeimarika zaidi.
Lakini kuanzia wakati huu hadi mwezi huu wa Desemba thamani ya shilingi imedorora kwa kima cha asilimia 10 dhidi ya dola ya Amerika. Kiwango hicho cha kudorora kwa thamani ni juu hata zaidi dhidi ya sarafu zingine kama vile Euro na Pauni ya Uingereza.
Thamani ya Shiling imepungua kutokana na kuongezeka kwa hitaji la dola ya Amerika baada ya fedha za kigeni zinazoingia nchini kupungua wakati ambapo bidhaa nyingi zinaingizwa nchini. Hii ni baada ya kulegezwa kwa masharti ya kudhibiti msambao wa Covid-19
Kudorora huku kwa thamani ya shilingi kutasababisha matatizo mengi kwa Wakenya kwa sababu bei ya magari na mafuta itapanda.
Kufikia Ijumaa Desemba 11, 2020 dola moja ya Amerika ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh111.54 kutoka Sh110 mwezi Novemba.