• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Somalia yakatiza uhusiano wa kidiplomasia na Kenya

Somalia yakatiza uhusiano wa kidiplomasia na Kenya

Na MASHIRIKA

NAIROBI, KENYA

SERIKALI ya Somalia imekatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na taifa la Kenya huku mgogoro kati ya mataifa haya mawili jirani ukizidi kutokota.

Taifa la Somalia limewaamrisha mabalozi wake wote kurejea nyumbani kutoka Nairobi na kuwapa mabalozi wa Kenya muda wa siku saba kuondoka nchini humo.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Mawasiliano wa Somalia Osman Abukar Dubbe kupitia vyombo vya habari nchini humo.

“Serikali ya Somalia kuambatana na hadhi yake kitaifa inayohakikishiwa na sheria na utaratibu wa kimataifa, na kwa kutimiza wajibu wake kikatiba kulinda utaifa, umoja na uthabiti wa nchi, imeamua kukatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na serikali ya Kenya,”

“Somalia inawaagiza mabalozi wake wote kurejea kutoka Kenya na kuwaamrisha wanadiplomasia wa Kenya kuondoka Somalia katika muda wa siku saba zijazo,” Dubbe alisema.

Tangazo hilo lilijiri baada ya Somalia kuwasilisha barua ya malalamishi dhidi ya Kenya kwa Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok, ambaye ndiye mwenyekiti wa Mamlaka ya Maendeleo kuhusu Ushirikiano baina ya Mataifa ya (IGAD) katika eneo hili.

Aidha, hatua hiyo imejiri huku Rais Uhuru Kenyatta akimpokea Rais wa taifa lililojitangaza kama Jamhuri ya taifa la Somaliland, Muse Bihi.

Somaliland ilitangaza uhuru kutoka nchi ya Somalia mnamo 1991 lakini haijatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) au nchi nyingine yoyote.

Hivi majuzi, Somalia iliishutumu Kenya kwa kuingilia masuala yake ya ndani.

Uhusiano kati ya Kenya na Somalia umeandamwa na uhasama unaozidi kuongezeka kutokana na masuala yanayosababisha migawanyiko kuhusu usalama na mpaka wa eneo la majini kati ya mataifa haya mawili ya Afrika Mashariki.

Mwezi uliopita, Somalia ilimfurusha balozi wa Kenya na kumrejesha balozi wake kutoka Nairobi baada ya kudai kwamba taifa hilo jirani lilikuwa linaingilia mchakato wa uchaguzi katika eneo la Jubbaland, ambalo ni miongoni mwa maeneo matano yanayoyotawaliwa na Somalia.

Hii si mara ya kwanza ambapo kumekuwa na uhasama kati ya Mogadishu na Nairobi.

Mwaka 2019 Kenya ilimrejesha balozi wake baada ya Mogadishu kuamua kunadi maeneo ya gesi na mafuta katika mzozo wa kimaeneo.

Nchi hizi mbili zilirejesha mahusiano yake miezi michache baadaye.

Kenya inachangia vikosi vya kijeshi nchini Somalia kama sehemu ya kikosi cha kudumisha amani kinachoongozwa na Umoja wa Mataifa ambacho, pamoja na serikali ya Somalia, kinapigana na kundi la wanamgambo waliojihami la al-Shabab linalohusishwa na al-Qaeda.

You can share this post!

FIDA yalia dhuluma nyumbani zimezidi

MWALIMU KIELELEZO: Millicent Achieng wa Shule ya Msingi ya...