• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Maafisa wa CDF wajuta kumeza hongo

Maafisa wa CDF wajuta kumeza hongo

Na TITUS OMINDE

MAHAKAMA moja mjini Eldoret inatarajiwa kuhukumu maafisa wawili wa hazina ya maendeleo katika eneobunge la Likuyani, Kaunti ya Kakamega baada ya kupatikana na hatia ya kupokea hongo. 

Mahakama ilikuwa imeambiwa kuwa wawili hao waliitisha hongo ya Sh50,000 kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule moja katika eneo bunge hilo kabla ya kutoa hundi ya hazina hiyo kwa mradi wa maendeleo shuleni mwake.

Wycliffe Shipwakula na  Susan Njeri  walishtakiwa kwa kupokea hongo ya Sh20,000 kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya St Peter’s Boys, Bw Samuel Akweyu mnamo Julai 14, 2014  kama kiinua mgongo kabla ya kumpa hundi  ya shule yake kutoka kwa hazina hiyo.

Bw Akweyu aliripoti kisa hicho katika afisi za maafisa wa tume ya maadili na ufisadi (EACC) mjini Eldoret waliompa Sh20,000 zenye alama ambazo zilitumika kunasa wawili hao.

Bw Akweyu, ambaye ni shahidi mkuu katika kesi hiyo aliambia mahakama kuwa wawili hao walikuwa na mazoea ya kuitisha hongo kabla ya kutoa hundi ya CDF kwa walimu wakuu  katika eneo hilo.

“Walitaka niwape hongo ya Sh50,000 kabla ya kunipatia hundi ya Sh1 milioni za maendeleo shuleni mwangu. Niliwaripoti kwa maafisa wa EACC ambao walinipa pesa zenye alama zilizotumika kama mtego kwao,” alisema Bw Akweyu.

Wawili hao ambao wamekuwa nje kwa dhamana. Akitoa uamuzi wa mahakama, hakimu mkuu wa Eldoret alisema kuwa wawili hao walipatikana na hatia hivyo basi watahukumiwa Jumatatu.

“Kutokana na ushahidi ambao umewasilishwa hapa kortini, ni bayana kwamba mmepatikana na hatia, mtajitetea Jumatatu kabla ya kuhukumiwa,” alisema hakimu,

 

 

 

You can share this post!

Wanachuo kutuzwa mamilioni kwa kuhimiza Wakenya kula wadudu

UTAMADUNI: Vazi la kumtawaza Ruto lazua mvutano wa wazee

adminleo