• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Kiini cha kufifia kwa nguvu za kufanya mapenzi

Kiini cha kufifia kwa nguvu za kufanya mapenzi

Na LEONARD ONYANGO

WENGI wa wanaume walio na tatizo la nguvu za kiume hupendelea kusalia kimya kwani huona aibu kulizungumzia au kwenda hospitalini kutafuta matibabu.

Tafiti zinaonyesha kuwa tatizo la kufifia kwa nguvu za kiume huongezeka umri unapoongezeka.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 50 ya wanaume wa umri wa miaka 50 na zaidi wanakumbwa na tatizo la nguvu za kiume lakini huwa ni vigumu kwao kulizungumzia au kwenda hospitalini kutafuta matibabu.

Wanaume walio na tatizo hili, wanakosa nguvu za kiume au wanadumu chini ya dakika tano wakati wa kufanya mapenzi.

Tatizo la nguvu za kiume linaweza kusababisha ndoa kusambaratika.Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa asilimia 42 ya wanawake huhisi kwamba wao ndio wamesababisha waume zao kukosa nguvu za kiume.

Asilimia 12 ya wanawake huhisi kwamba hawapendwi au wamepuuzwa waume zao wanapopatwa na tatizo la nguvu za kiume.Wanaume wengi wanapopatwa na tatizo hili huamua kutumia uchovu kama kisingizio cha kutoshiriki tendo la ndoa na wake zao.

Baadhi ya wanaume huamua kunyamaza bila kuwaambia wake zao kinachoendelea.Dkt Joachim Osur, mkurugenzi wa Afya ya Uzazi wa Amref, anasema kuwa kufifia kwa nguvu za kiume kunaweza kuwa dalili za maradhi ya moyo.

“Mtu yeyote aliye na matatizo ya nguvu za kiume anafaa kutafuta huduma za matibabu ya haraka ili kuepuka kifo cha ghafla kinachosababishwa na maradhi ya moyo,” anasema Dkt Osur.

Anasema kuwa tatizo hili linaweza kutibiwa iwapo mwathiriwa atatafuta matibabu ya haraka.Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), uvutaji wa sigara unaweza kusababisha mwanaume kupoteza nguvu za kiume.

Kuwa na mafuta mengi mwilini haswa maeneo ya kiunoni, unene kupindukia, msongo wa mawazo, ubugiaji wa pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, kuzibika kwa mishipa ya damu ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kusababisha nguvu za kiume kudorora. Dkt Osur anasema kuwa baadhi ya vyakula vinaweza kuimarisha nguvu za kiume.

Baadhi ya vyakula anavyopendekeza ni matunda, mboga, nafaka na mbegu. Vyakula hivyo vinasaidia damu kutiririka katika viungo vyote vya mwili hadi katika sehemu nyeti. Mboga zinazoweza kusaidia ni kama vile Sukumawiki, spinachi na karoti. Matunda yaliyo na manufaa zaidi ni ndizi na tofaa (apple).

Mbegu kama vile maharagwe na njugu pia zinasababisha mwanaume kuwa na makali. Vyakula vingine ni viazi, kuku, mayai, maziwa na parachichi.

Kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka pombe, sigara na mambo yanayosababiosha msongo wa mawazo pia kunasaidia mwanaume kutoishiwa na nguvu za kiume.

You can share this post!

Dawa bandia za hamu ya mapenzi zinavyohatarisha maisha ya...

Wakenya wasafiri mashambani licha ya onyo la serikali