Habari Mseto

Masharti ya usafiri ?yaimarishwa Lamu

December 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

MADEREVA wa magari ya usafiri wa umma watakaokaidi masharti yaliyowekwa kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa ili kuzuia mashambulizi ya Al-Shabaab watakamatwa na kushtakiwa.

Idara ya Usalama, Kaunti ya Lamu, imewaonya vikali madereva na abiria hao, hasa wale ambao wamekuwa wakiendeleza kisiri safari za usiku na pia kuepuka msafara wa magari unaosindikizwa na polisi kwamba siku zao zimehesabiwa.

Jumatatu, wadau wa usalama, kaunti ya Lamu waliandaa kikao cha dharura ili kujadili jinsi mpangilio wa usafiri utakavyotekelezwa kwenye barabara kuu ya Lamu hadi Mombasa hasa msimu huu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Kikao hicho pia kilichochewa na jaribio la Al-Shabaab kuteka nyara gari la polisi wa kushika doria mipakani (BPU) katika eneo la Nyongoro mnamo Jumapili.

Akizungumza na Taifa Leo Jumanne, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema kuna baadhi ya madereva na wamiliki wa magari ya usafiri wa umma ambao wamekuwa wakikiuka mikakati iliyopo ya usalama.

Alisema tayari wameanzisha msako kwa wale wanaokaidi masharti husika na kwamba hivi karibuni watawatia mbaroni na kuwashtaki wahusika hao.

Alishikilia kuwa marufuku ya kutosafiri usiku kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa bado ipo na kwamba yafaa kuheshimiwa.Marufuku hiyo iliwekwa tangu Julai, 2014 baada ya visa vya magari ya usafiri wa umma na yale ya polisi kushambuliwa na abiria na walinda usalama kuuawa kiholela na Al-Shabaab kukithiri kwenye barabara hiyo.

Miongoni mwa watakaoathirika moja kwa moja na masharti mapya ni wamiliki wa matatu almaarufu Shuttle ambao mara nyingi wamekuwa wakisafirisha abiria kutoka jeti ya Mokowe Kaunti ya Lamu hadi Mombasa majira ya asubuhi kupita kiasi ili kuepuka msafara wa magari unaosindikizwa na polisi na ambao wanahisi unachelewesha shughuli zao.

“Tumekuwa na kikao kujadili hali ya usafiri kwenye barabara ya Lamu hadi Mombasa msimu huu wa sherehe. Tumeafikia kukaza kamba zaidi hasa kuhusiana na masharti yaliyopo ya usafiri kwenye barabara yetu. Kwa sasa kila gari la usafiri wa umma litahitajika kusubiri msafara ili yasindikizwe na maafisa wa polisi. Isitoshe, wale ambao wamekuwa wakiendeleza safari za usiku kisiri pia wakome. Huko ni kuhatarisha maisha ya abiria na hata wewe dereva mwenyewe. Tukikupata tutakukamata na kukushtaki,” akasema Bw Macharia.

Aidha kufuatia shambulizi la Jumapili, Bw Macharia alisema tayari wameongeza doria za walinda usalama kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa kwa masaa yote 24.

Kamishna huyo pia alifichua kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama kwenye vituo vyote vilivyobuniwa kando ya barabara hiyo, ikiwemo Ndeu, Milihoi, Mambo Sasa, Lango la Simba na Gamba ili kuzuia mashambulizi ya Al-Shabaab.Alisema msako mkali wa kuwatafuta magaidi wa Al-Shabaab kwenye eneo la Nyongoro na viungani mwake bado unaendelea japo hawajanasa mhalifu yeyote hadi sasa.

“Mbali na kukazia kamba masharti ya usafiri barabarani, pia tumeongeza doria za walinda usalama wetu, ikiwemo polisi na wanajeshi (KDF) maeneo haya. Utapata polisi na KDF wakipitapita barabarani masaa yote ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara yetu unadhibitiwa vilivyo. Operesheni ya kuwasaka Al-Shabaab eneo la Nyongoro na viungani mwake pia inaendelea. Wananchi wasiwe na shaka,” akasema Bw Macharia.