• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
TAHARIRI: Kurudisha kodi ni pigo kwa Wakenya

TAHARIRI: Kurudisha kodi ni pigo kwa Wakenya

NA MHARIRI

HATUA ya serikali ya kupunguza kodi za bidhaa (VAT) na mapato (PAYE) na ushuru kwa kampuni mnamo Aprili mwaka huu iliwafaidi wafanyabiashara na waajiri na wamiliki wa kampuni.

Katika afueni iliyotolewa na serikali Aprili, ushuru huo ulipunguzwa hadi kima cha asilimia 25. Lakini jana Rais Uhuru Kenyatta alitia saini mswada wa Kodi ya Mapato, unaotaka kurejesha hali kuwa kama zamani.

Japokuwa si mara ya kwanza kuzungumzia jambo hili, lina umuhimu mkubwa kwa maisha ya mwananchi wa chini.Jana na leo, mamia ya wananchi wamekwama kwenye vituo vya magari wakijaribu kwenda kwao mashambani. Sababu kubwa ya wao kukwama ni kukosekana kwa magari kutokana na kuwa lazima wakae watu wanane pekee.

Tahariri hii haina lengo la kuunga mkono sekta yoyote ya uchumi, lakini mbona bai kama serikali inaona mambo yameanza kuwa ya kawaida, matatu zinaendelea kubeba asilimia 60 ya abiria?

Walipokuwa wakiwasilishwa mswada huo Jumanne, wabunge walidai kuwa lengo si kuwaumiza wananchi bali kuwasaidia kwa kuiwezesha serikali kuongeza mapato yake ili iweze kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kulipa mishahara.

Kwamba wafanyabiashara hawapasi kuongeza bei za bidhaa kwa sababu kimsingi viwango vya ushuru havijaongezwa.

Kupitishwa kwa sheria hiyo kuna maana kuwa kuanzia Januari mosi, gharama ya maisha itaanza kupanda isipokuwa kwa waajiriwa wanaopokea mishahara ya chini ya Sh24,000 kwa mwezi.

Ni kweli kuwa uchumi wa Kenya uko katika ICU. Kwamba mzigo wetu wa madeni umefikia Sh7 trilioni na kiwango hicho kinaendelea kupanda.

Lakini kurejesha ushuru wa kitambo wakati watu hawana ajira, biashara hazijaimarika na hakuna uchumi wa saa 24, ni kuwa na ubinafsi.Ingawa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) itafurahia kukusanya mabilioni, wafanyabiashara wataongeza bei za bidhaa ili kuziba hasara itakayotokana na ongezeko hilo la ushuru. Mzigo huo atabebeshwa mnunuzi na mtumiaji huduma.

Kwa vile tayari Rais ameupitisha mswada huo kuwa sheria, kinachohitajika kwa sasa ni mpango maalum wa kuwafaa Wakenya ambao hawajarejelea hali ya kawaida kimaisha. Pesa zitakazokusanywa, zisimamie elimu bila malipo katika shule zote – za umma na kibinafsi.

You can share this post!

Misongamano mijini wananchi wakielekea mashambani kwa...

FAUSTINE NGILA: Shirika la Utafiti wa Angani limezembea...