• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
SAKATA YA NYS: Nyavu za Kinoti na Haji zavua dagaa, zalemewa na Tilapia

SAKATA YA NYS: Nyavu za Kinoti na Haji zavua dagaa, zalemewa na Tilapia

Na VALENTINE OBARA

ORODHA ya washukiwa watakaoshtakiwa kwa madai ya kuhusika kwenye kashfa ya ufisadi katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ina idadi kubwa ya wafanyakazi wa ngazi za chini serikalini na taasisi hiyo, hali iliyozua maswali kuhusu walipo wahusika wakuu.

Orodha hiyo iliyotolewa Jumatatu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji (pichani), ina majina 40 ya watumishi wa umma, 14 ya wakurugenzi wa biashara na 10 ya kampuni za kibiashara ambazo zinaaminika zilihusika katika sakata hiyo ya ufujaji wa pesa za umma.

Watumishi wa umma wa ngazi za juu zaidi katika orodha hiyo ni Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Kijinsia Bi Lilian Omollo, Mkurugenzi wa NYS Richard Ndubai na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NYS Sammy Michuki.

Mbali na wasimamizi na wakurugenzi wachache wa idara mbalimbali za NYS na Wizara ya Fedha kama vile idara za uchukuzi na uhasibu, kuna msimamizi wa stoo wa NYS, mtahini, watengenezaji bili za kununua bidhaa na wafanyakazi ambao haijatambuliwa wanafanya kazi gani.

Rais Uhuru Kenyatta jana alirejelea msimamo wake kwamba serikali haitavumilia kuwa na watumishi wa umma ambao ni watovu wa maadili.

“Watu waliotwikwa majukumu lazima wawe tayari kutumikia umma na wala si kutumikiwa,” akasema, na kuongeza kuwa uadilifu hauhusu tu mamlaka makubwa serikalini bali jinsi waliotwikwa mamlaka wanavyoitumia.

Kulingana na Bw Haji, akaunti za watu wote waliotajwa zimezufungwa. Alisema upelelezi unaoendelezwa utapanuliwa ili kuchunguza pia biashara zingine ambazo inaaminika pesa hizo ziliwekezwa kwao.

 

 

You can share this post!

NYS yafaa kuvunjwa na fedha hizo kufadhili elimu –...

SAKATA YA NYS: Wakenya watamauka wakisema washukiwa...

adminleo