• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
SAKATA YA NYS: Wakenya watamauka wakisema washukiwa watajinasua kama kawaida

SAKATA YA NYS: Wakenya watamauka wakisema washukiwa watajinasua kama kawaida

Na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Wakenya wasema wamezoea kuona wahusika kwenye wizi wa mabilioni ya pesa za umma katika miaka ya awali wakiwa huru wakifurahia utajiri wa wizi
  • Hakuna aliyechukuliwa hatua kwenye sakata za ufisadi kama Goldenberg, Anglo Leasing, wizi ndani ya Wizara ya Afya, mahindi, ununuzi wa vifaa vya uchaguzi vya IEBC (Chickengate), na sakata ya kwanza ya NYS 
  • Kesi kuhusu baadhi ya sakata hizo zimeendelea kwa miaka mingi na kuzima matumaini ya Wakenya kwamba wahusika wataweza kuadhibiwa, huku washukiwa wakuu wakijinasua
  • Noordin Haji Jumatatu alisema idara yake imezindua mwanzo mpya katika vita dhidi ya ufisadi na akahakikishia Wakenya kwamba waliomeza mabilioni bila jasho watakiona 

WASHUKIWA 20 wa ufisadi katika sakata ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) walikamatwa jana na wengine 34 wanasakwa.

Lakini kukamatwa huko kulipokelewa na Wakenya kwa hali ya kukata tamaa wakisema hii ni sarakasi ambayo inajirudia sawa na kashfa za awali za wizi wa pesa za umma.

Waliohojiwa na Taifa Leo hawakuonekana kuchangamkia msako wa Jumatatu wakisema wamezoea matukio hayo, ambapo wahusika kwenye wizi wa mabilioni ya pesa za umma katika miaka ya awali wangali huru na wanaendelea kufurahia utajiri wa wizi.

Matukio yaliyopelekea maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kukamata washukiwa wanaodaiwa kuhusika katika ufujaji wa takriban Sh0.5 bilioni za NYS yalifuata mtindo sawa ambao umekuwa ukishuhudiwa kwenye kashfa za awali.

Sawa na kashfa za awali, sakata ya NYS ilifichuliwa na vyombo vya habari, ikafuatia miito kutoka kwa wanasiasa na mashirika ya kijamii kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika, kamati husika ya bunge ikahoji washukiwa wakuu nayo DCI ikawakamata.

Jumanne wanatarajiwa kushtakiwa, na hapo ndipo kashfa za awali zimekwama, na wengi wanauliza iwapo hii itafuata mkondo huo huo.

Hii haikutofautiana na sakata za ufisadi kama vile Goldenberg, Anglo Leasing, ununuzi wa kliniki tamba katika Wizara ya Afya, ununuzi wa vifaa vya uchaguzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (Chickengate), na sakata ya kwanza ya NYS iliyotokea mwaka wa 2015.

Kesi kuhusu baadhi ya sakata hizo zimeendelea kwa miaka mingi na kuzima matumaini ya Wakenya kwamba wahusika wataweza kuadhibiwa, huku washukiwa wakuu wakifanikiwa kujiondolea lawama.

“Ni lazima serikali idhihirishe imejitolea kikamilifu kupambana na ufisadi kwa kuadhibu wahusika wakuu. Katika sakata iliyopita ya NYS wapelelezi walilenga watu wadogo ndiposa hapakuwa na mafanikio waliposhtakiwa,” akasema Mwenyekiti wa National Youth Sector Alliance (NYSA), Emmanuel Ngongo.

Sawa na jinsi ilivyokuwa katika miaka iliyotangulia, maafisa wakuu wa NYS walitangaza kujiuzulu kwa muda ili kutoa nafasi ya uchunguzi kukamilishwa. Maafisa hao ni Mkurugenzi Mkuu Richard Ndubai, na Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Vijana Bi Lillian Mbogo-Omollo.

Usiku wa kuamkia Jumatatu, oparesheni iliyofanywa kukamata washukiwa hao haikutofautiana na za miaka iliyotangulia.

 

Ushahidi wa kutosha

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Jumatatu alisema idara yake imezindua mwanzo mpya katika vita dhidi ya ufisadi na akahakikishia Wakenya kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha watu walilipwa pesa bila kutoa huduma wala bidhaa zozote kwa NYS.

“Tuna ushahidi wa kutosha katika kesi hii,” alisema Bw Haji.

“Tunavyojaribu kufanya sasa ni kubadilisha mienendo iliyokuwepo mbeleni. Ufisadi ni kitu ambacho kimeumiza sana nchi hii kiuchumi na katika sekta mbalimbali.

Ingawa itachukua muda kuangamiza ufisadi nataka kuhakikishia Wakenya kwamba huu ni mwanzo mpya wa vita dhidi ya ufisadi.”

Washukiwa wamehusishwa na ufujaji wa pesa uliotokea kuanzia mwaka wa 2013 na miongoni mwa mashtaka yatakayowakumba ni kupanga njama ya kutenda ufisadi, kuzembea katika majukumu yao, utumizi mbaya wa mamlaka na kupokea fedha kwa njia haramu.

You can share this post!

SAKATA YA NYS: Nyavu za Kinoti na Haji zavua dagaa,...

SAKATA YA NYS: Benki sita kuchunguzwa zilivyosaidia wizi wa...

adminleo