• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Tutatwaa mabilioni yote ya wizi, aahidi Uhuru

Tutatwaa mabilioni yote ya wizi, aahidi Uhuru

Na VALENTINE OBARA

WASHUKIWA wa ufisadi watakaopatikana na hatia watapokonywa mali zote walizojizolea kutokana na uporaji wa mali ya umma, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Jumatano.

Akihutubu katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi, kwenye hafla ya kukabidhi wananchi hati miliki za ardhi, rais aliwaonya watu wanaofuja mali ya umma wakome kutumia makabila yao kujitetea akisema serikali itahakikisha mali walioiba imerudishwa kwa wananchi.

“Wale ambao wataendelea kucheza na mali ya wananchi wajue siku zao zimehesabiwa na ni shida watapata. Tumesema kutoka sasa hatutaki kusikia mtu akitetea mwenzake eti mtu akiiba anasema ni kabila langu au dini yangu inadhulumiwa. Wewe ulliba peke yako, beba msalaba wako peke yako,” akasema.

Rais alizungumza siku moja baada ya washukiwa 24 wa ufisadi katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kufikishwa mahakamani ambako walikanusha mashtaka mbalimbali na kuzuiliwa hadi Juni 5.

Wakati huo huo, mabalozi wa nchi za magharibi wametaka serikali isipendelee yeyote atakayethibitishwa alihusika katika ufisadi.

Mabalozi hao 18 jana walisema nchi zao zimejitolea kusaidia Kenya kupambana na ufisadi lakini mafanikio yatapatikana tu ikiwa Wakenya wote wataungana na kuchukua hatua zinaostahili bila mapendeleo.

“Hakuna nchi ambapo hakuna ufisadi na nyingi kati ya zetu zimekumbwa na changamoto,” wakasema kwenye taarifa.

Mabalozi waliotia saini taarifa hiyo ni Robert Godec (Amerika), Nic Hailey (Uingereza), Stefano Dejak (Muungano wa Ulaya), Mette Knudsen (Denmark), Anna Jardfeldt (Sweden), Ralf Heckner (Uswizi) na Frans Makken (Uholanzi) miongoni mwa wengine.

 

You can share this post!

Uhuru: Mimi si mtu wa kutishwatishwa na yeyote

Tahadhari Al Shabaab wanapanga shambulio

adminleo