• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Mbunge aonya wakazi dhidi ya kufurahia mlo wa nyama ya tumbili

Mbunge aonya wakazi dhidi ya kufurahia mlo wa nyama ya tumbili

Na KNA

MBUNGE Mwanamke wa Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege, ameonya wakazi wa kaunti hiyo dhidi ya kula nyama ya tumbili akisema wanaweza kuambukizwa magonjwa hatari kama Ebola.

Kumekuwa na ripoti kuhusu wakazi wanaokula tumbili ambao wamekuwa wakiharibu mimea eneo hilo.

Akizungumza kwenye mkutano katika makao makuu ya kaunti, mbunge huyo alisema ulaji wanyama hao haufai kuchukuliwa kwa mzaha kwa kuwa kuna hatari kubwa kwa afya ya binadamu.

Alisema tumbili wanafahamika kusheheni virusi vinavyosababisha magonjwa hatari kama vile Ebola ambayo imesababisha maafa mengi katika nchi tofauti, ikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo ambako ugonjwa huo unaenea kwa sasa.

Bi Chege alisema, wananchi wanafaa wahamasishwe kuhusu hatari ya uraibu huo. “Watu wetu hawafai kuchukulia suala hili kimzaha,” akasema Bi Chege, na kuongeza kuwa maeneo husika yanafaa yatambuliwe ili hatua muafaka zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Kulingana na shirika la utafiti wa kimatibabu la Center for Disease Control and Prevention (CDC), tumbili huweza kuambukiza binadamu magonjwa hatari kama vile Ebola, Monkey B Virus na Monkey Pox.

You can share this post!

KNEC yaonya kuhusu hatari ya wizi wa mitihani kurudi

Simanzi mvulana kufariki akiokoa mbwa wake mtoni

adminleo