Kalonzo, Mudavadi na Weta wapinga kubuniwa kwa jopo la kuzima ufisadi
Na VALENTINE OBARA
VINARA watatu wa Muungano wa NASA wamejitenga na msimamo wa mwenzao Raila Odinga, kuhusu vita dhidi ya ufisadi.
Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Jumatano walipinga pendekezo la kubuniwa kwa jopokazi maalumu la kupambana na ufisadi nchini.
Pendekezo hilo lilikuwa limetolewa mwishoni mwa wiki na Bw Odinga ambaye uhusiano wake wa kisiasa na watatu hao umeonekana kudorora tangu alipoamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta miezi miwili iliyopita.
Kwenye taarifa ya pamoja, watatu hao walisema asasi za kupambana na ufisadi zilizopo kwa sasa zinahitaji tu kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kupewa uhuru wa kutosha ili zifanikiwe kuangamiza janga hilo sugu.
“Huu si wakati wa kuunda taasisi nyingine kwa minajili ya kupambana na ufisadi. Kuunda taasisi inayofanana na zile zilizopo na kuchukua hatua za kisiasa kutachangia tu kuficha wahusika wakuu, kutoa nafasi zaidi ya wahusika kupeana bakshishi na kuadhibu tu wahusika wadogo,” wakasema.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa vinara hao kutoa taarifa ya pamoja kuhusu ufisadi nchini baada ya sakata mpya kufichuliwa katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wiki chache zilizopita.
Tofauti na jinsi ilivyokuwa wakati Bw Odinga alipokuwa akishirikiana pamoja na watatu hao, upande wa upinzani umeonekana kukosa makali ya kushinikiza serikali ibadilishe mienendo yake inapokosea.
Mbali na kumpinga kiongozi huyo wa Chama cha ODM, watatu hao pia walikosoa hatua zilizochukuliwa na serikali kufikia sasa kupambana na ufisadi. Kulingana nao, serikali haijadhihirisha kujitolea kukamata wahusika wakuu wanaopora mali ya umma licha ya kutoa ahadi za kufanya hivyo mara kwa mara.
“NASA itaamini serikali imejitolea tu ikiwa wale walio na ushawishi ndani na nje ya serikali watapelekwa mahakamani kwa msingi wa ushahidi wa kutosha ili wafungwe, na wala si sarakasi tunazoshuhudia ambapo washtakiwa ni mawakala tu,” wakasema.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DPP) ilipeleka washukiwa 24 wa ufisadi wa NYS mahakamani Jumanne ingawa wengi wao ni watu wa vyeo vya chini isipokuwa Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo-Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai.