• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
SAKATA YA NYS: Watuhumiwa zaidi wajisalimisha kwa polisi

SAKATA YA NYS: Watuhumiwa zaidi wajisalimisha kwa polisi

Na SAM KIPLAGAT

WASHUKIWA zaidi wa kashfa ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), Jumatano walijisalimisha kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), huku upande wa mashtaka ukiendelea kutayarisha mashtaka kwa watu 40 na kampuni zilizotajwa kwenye sakata hiyo.

Hakimu Mkuu Douglas Ogoti alikuwa amewapa washukiwa hao hadi jana saa nane kujiwasilisha kwa DCI. Alikataa ombi la mawakili wao waliopinga agizo hilo.

Kulingana na mawakili hao, washukiwa walifaa kufika mbele ya mahakama wakisema kufika mbele ya wapelelezi kungefanya wazuiliwe hadi Jumatatu.

“Baadhi ya washukiwa walio mbele ya mahakama wamekuwa wakizuiliwa kwa zaidi ya saa 24. Tunashuku wanataka kuwazuilia hadi Jumatatu ikizingatiwa kuwa Ijumaa ni siku kuu,” wakili Cliff Ombetta aliyemwakilisha Wellington Lubira aliambia mahakama.

Washukiwa wengine ambao hawakuwa kortini ni Clara Mbao, Peter Muthomi Muguongo, Simon Kanyi Kairu, Ezekiel Ombaso Osoro na Julius Airo. Wengine walikuwa Michael Ojiambo, Peter Waema, na George Otieno miongoni mwa wengine.

Wakili Kirathe Wandugi, ambaye aliwakilisha washukiwa kadhaa alidai kwamba kuwataka kujiwasilisha kwa wapepelezi ni kuwatisha na kuwaadhibu. Mahakama iliambiwa kwamba baadhi ya washukiwa walijipeleka kwa DCI lakini wakafukuzwa. Waliokuwa kortini Jumanne ni pamoja na Katibu wa Kudumu wa masuala ya vijana Lillian Mbogo Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai.

Wengine ni Sammy Michuki, Sophy Karimi, Rodgers Nzioka, Evan Wafula Kundu, Welenalo Mulupi, Ferdinand Matano Odonyo, Christopher Malala na Sammy Mbugua Mwangi.

Wafanyabiashara Anne Wanjiku Wambere Ngirita, Lucy Wambui Ngirita, Phyllis Ngirita, Simon Kanai, James Katululu na Jeremiah Ngirita ni miongoni mwa walioshtakiwa na kuzuiliwa rumande hadi Juni 5 mahakama itakapoamua iwapo wataachiliwa kwa dhamana.

You can share this post!

SAKATA YA NYS: Washukiwa 24 kusalia ndani kwa siku 7

Gideon Moi apewa mwezi mmoja kugura ofisi ambayo alitengewa

adminleo