Kundi la kwanza la madaktari wa Cuba latua nchini
Na AGGREY OMBOKI
KUNDI la kwanza la madaktari kutoka Cuba liliwasili nchini Jumanne usiku. Ndege ya KLM iliyokuwa imewabeba madaktari hao ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa tatu na dakika 47.
Kuwasili kwao kunatimiza mkataba uliotiwa saini baina ya Kenya na Cuba kuruhusu madaktari 100 spesheli kutoka taifa hilo la Caribbean kuja nchini kufanya kazi kwa kandarasi.
Mpango huo umeshutumiwa vikali na madaktari wa humu nchini.
Madaktari hao wa Cuba walilazimika kusubiri kwa zaidi ya saa mbili kukamilisha taratibu za idara ya uhamiaji kwa abiria wanaowasili kwenye uwanja huo.
Baada ya ukaguzi walifululizwa hadi mabasi yaliyokuwa yakiwasubiri na kuondoka mara moja.
Walipokewa na Naibu Waziri wa Afya Rashid Aman, Mkurugenzi wa Matibabu Jackson Kioko na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o.
Kundi la pili la madaktari linatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi, Juni 7, 2018.
Dkt Aman alisema matabibu hao watapokea mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Serikali ili kupata ufahamu wa mfumo wa matibabu humu nchini.
Alieleza: “Madaktari hao watapokea mafunzo jinsi mfumo wetu wa matibabu hufanya kazi kabla kutumwa katika vituo mbalimbali vya afya katika kaunti kadha.
“Lengo kuu la kuwaleta madaktari hawa ni kujifunza kutokana na tajriba ya Cuba ya kukuza mfumo imara wa matibabu ambao umewezesha taifa hilo kutoa huduma za matibabu za bei nafuu kwa wananchi wote.”
Kwa upande wake, alieleza naibu waziri, Kenya itatuma madaktari wake 50 nchini Cuba ili kupokea mafunzo katika tiba ya familia.
“Kama sehemu ya mkataba wa makubaliano tuliotia saini na Cuba, tutatuma madaktari wettu 50 ili wakajifunze kuhusu mfumo wa matibabu wa Cuba ambao umewezesha kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wake wote. Kundi hilo litajumuisha daktari mmoja kutoka kila kaunti zote 47,” akasema.
Dkt Aman aliwaomba Wakenya kuwapa fursa madaktari hao kufanya kazi licha ya shutuma nyingi zilizotolewa.
“Kumekuwa na habari hasi kuhusu mkataba lakini tunaamini madaktari hao wako na jukumu muhimu la kutekeleza katika mfumo wetu wa matibabu.”