Habari Mseto

Wanaharakati wapinga uchimbaji wa makaa ya mawe Lamu

June 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

KALUME KAZUNGU na WYCLIFFE MUIA

WANAHARAKATI Jumanne waliandamana jijini Nairobi kupinga uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe (coal) katika kaunti za Kitui na Lamu.

Waandamanaji hao walitaja madini hayo kama ‘sumu’ kwa kaunti za Kitui na Lamu ambapo uchimbaji wa makaa hayo unatarajiwa kuanza. “Sisi si wajinga! Tunakataa uchimbaji wa makaa ya mawe katika kaunti za Lamu na Kitui,” wanaharakati hao waliimba huku wakiandamana hadi Bunge la Kitaifa kuwasilisha malalamishi yao.

Wabunge watatu wamepinga vikali mpango wa Gavana wa Kitui Charity Ngilu kuruhusu uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo la Mui, kaunti ndogo ya Mwingi ya Kati

Mbunge wa Mwingi ya Kati, Gideon Mulyungi na mwenzake wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai walisema wakazi wa eneo hilo hawajahusishwa katika mpango huo. Naye mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kitui Irene Kasalu, alisema sharti tahadhari ichukuliwe kabla ya mpango huo kuanza.

Katika Kaunti ya Lamu, wanaharaki wameonya vikali serikali dhidi ya kutekeleza mradi wa Sh200 bilioni wa nishati ya makaa ya mawe eneo hilo, wakiutaja mradi huo kuwa sumu kwa mazingira.

Wanaharakati hao kutoka miungano ya Save Lamu, Lamu Youth Alliance, Lamu Marine Forum na ule wa uhifadhi wa mazingira, wanyama pori na viumbe wa majini walisema huku Kenya ikiungana na mataifa mengine katika kuadhimisha hafla ya mazingira ulimwenguni, kuna haja ya serikali kutupilia mbali miradi ya kawi ambayo ina athari kubwa kwa mazingira na afya ya wakazi nchini.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Save Lamu,Walid Ahmed, wanaharakati hao walisema hawatakoma kuishinikiza serikali kutupilia mbali miradi inayohatarisha mazingira nchini na ulimwenguni kwa jumla.

Bw Walid alisema huenda azma ya kuhifadhi mazingira safi nchini isiafikiwe ikiwa serikali itakubali miradi hatari kwa mazingira.