Jaji azima madaktari wa Cuba kuanza kuhudumu Kenya
Na MAUREEN KAKAH
HATIMA ya madaktari kutoka Cuba ambao walianza kuwasili nchini juzi kuhudumu Kenya, sasa iko mikononi mwa mahakama ambayo imeagiza wasipewe vibali vya kufanya kazi Kenya.
Hii ni baada ya Mahakama ya kutatua mizozo ya wafanyakazi kuwasimamisha kwa muda kuanza kazi hadi kesi ya kupinga hatua ya serikali ya kuwaleta nchini isikilizwe na kuamuwa Juni 19.
Jaji Onesmus Makau alitoa agizo hilo akisema kwa sababu mahakama haikuthibitishiwa kwamba madaktari hao watakuwa wameanza kazi kabla ya Juni 19, hali inafaa kubaki ilivyo hadi uamuzi utolewe tarehe hiyo.
“Kwa maoni yangu, itakuwa haki mahakama inapoandika uamuzi wake, pande zote zitulie na kuwa na subira,” alisema Jaji Makau.
Aliongeza: “Kwa sasa, madaktari kutoka Cuba ambao waliajiriwa kupitia mfumo unaopingwa hawajafika katika vituo vyao vya kazi, kwa hivyo watasubiri uamuzi wa korti.”
Dkt Samson Robert Misango, ambaye ni daktari kutoka Kenya ameshtaki Waziri wa Afya, Baraza la Magavana, Mkurugenzi wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu.
Dkt Misango anapinga mkataba kati ya serikali ya kitaifa, serikali 47 za kaunti na serikali ya Cuba ya kuwaleta wataalamu 100 wa afya kuhudumu nchini kuanzia Mei 30.
Analaumu serikali akidai imedanganya ulimwengu kwamba Kenya ina uhaba wa madaktari ilhali kuna madaktari wengi waliohitimu ambao hawana kazi.
Katika kesi yake anataka mahakama kuzuia idara ya uhamiaji kuwapa madaktari hao wa kigeni vibali vya kufanya kazi Kenya.
Kesi nyingine kuhusu suala hilo iliwasilishwa na Bw Samwel Nduati, Reuel Maina na Francis Thuku ambao wanadai hawana ajira. Watatu hao wanasema serikali inafaa kuwaajiri Wakenya waliohitimu kwanza kabla ya kuwaajiri raia wa kigeni.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Matibabu Dkt Jackson Kioko anatetea hatua ya serikali akisema iliwaleta madaktari hao nchini kwa sababu kuna uhaba wa madaktari.
Dkt Kioko aliambia mahakama kwamba madaktari 100 kutoka Cuba walichaguliwa kwa uangalifu na kuhojiwa ili kuthibitisha iwapo wamehitimu.
Alisema Wizara ya Afya na bodi ya kusimamia madaktari zilishiriki kuwachagua na kuwahoji madaktari hao.
Kundi la kwanza la madaktari 50 liliwasili nchini Jumanne na wengine walitarajiwa kuwasili jana.