• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:15 AM
KURUNZI YA PWANI: Mafuriko yaacha jamii na matatizo ya kiafya

KURUNZI YA PWANI: Mafuriko yaacha jamii na matatizo ya kiafya

WINNIE ATIENO Na STEPHEN ODUOR

MVUA kubwa ambayo ilisababisha mafuriko na maafa katika sehemu mbalimbali nchini, imeziacha familia nyingi zikikabiliana na kuathirika na matatizo ya kiafya.

Katika Kaunti ya Tana River ambayo ndio iliathirika zaidi na matatizo ya mafuriko huko Pwani baada ya shule na majumba kusombwa na maji wakazi wanakodolea macho mlipuko wa kipindupindu baada ya watu 78 kupatikana na ugonjwa huo hatari.

Majuzi mzee mmoja aliaga dunia katika kituo cha matibabu cha Madogo baada ya kupatikana na kipindupindu. Kulingana na afisa wa afya na usafi katika kaunti hiyo, Mwanajuma Hiribae ugonjwa huo umedhibitiwa.

“Wagonjwa 44 tayari wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani,” akasema Bi Hiribae.

Huko Mombasa maradhi yanayosambazwa na mbu ikiwemo homa kali ya dengue na chikungunya inaendelea kuwaathiri mamia ya wakazi huku wakiendelea kupokea matibabu katika hospitali za kibinafsi na zile za ugatuzi.

Kipindupindu husababishwa na aina ya bakteria aitwaye Vibrio cholerae ambayo inasambaa kwa haraka sana na hata kusababisha maafa. Ugonjwa huo ni wa kuambukizwa kupitia viini vinavyoenezwa kupitia kwa kinyesi kutoka kwa wagonjwa wenye kipindupindu.

Wagonwja wanaoathirika na ugonjwa huo hupata haja kubwa iliyo majimaji na kudhoofika haraka kwa sababu ya kukosa maji mwilini. Kipindupindu husambaa mahali kuliko na ukosefu wa maji ya mfereji au mabomba ya kupitisha maji machafu.

Watu hao walilazwa katika kituo cha afya cha Madogo wakiendelea kupokea matibabu.

Lakini tatizo la kipindupindu litaendelea kushamiri baada ya kaunti hiyo kukosa usambaziwa maji safi.

“Tunatumia maji ya mvuo iliyojaa katika vidimbwi ndio maana tunazidi kuathirika na kipindipindu sababu maji hayo si safi,” akasema Mzee Kalu kutoka eneo la Madogo.

Vijiji vinne vimeathiriwa na kipindupindu ikiwemo Bulavango, Bulakaratasi, Bulakodha na Madogo C.

Serikali ya kaunti inaendelea kuweka mikakati kuhakikisha ugonjwa huo hausambai au hata kusababisha maafa.

Akiongea na waandishi wa habari katika kituo cha afya cha Madogo Bi Hiribae alisema vijiji vinne vimeathirika.

“Wagonwja 78 wamelazwa katika kituo hiki wakiendelea kupokea matibabu. Tunashuku kuwa waathiriwa walikunywa maji taka ya mvua katika kidimbwi. Tunaendelea kupata visa vingi za kipindipindu kutokana na uhaba wa dawa za prophylactic katika hospitali zetu,” akasema Bi Hiribae.

Hata hivyo, aliwahakikishia wakazi kuwa serikali ya kaunti hiyo imeagiza dawa za kukabiliana na ugonjwa huo.

Kando na dawa, serikali ya kaunti itaanza kusambaza maji safi ili wakazi wasitumie maji chafu kutokana na maji taka mabombani.

“Tutakabiliana na uhaba wa maji ambayo inasababisha wakazi kutumia maji chafu. Tatizo la maji limetokana na mabomba ya maji yaliyoharibika kutokana na mafuriko. Tutarekebisha mabomba hayo katika huduma za maji za Madogo,” akaongeza.

Abdi Loka mkaazi wa Bura alisema serikali jirani ya kaunti ya Garissa iliitikia dharura hiyo na kuwapa huduma za afya.

“Tunashangaa serikali jirani ilitusaidia kwa haraka sana ikilingwanishwa na serikali yetu. Madaktari wa Garissa walifika na kutupa huduma za afya ilhali Tana River ni kaunti tofauti,” akaongeza.

Wakazi wa Mombasa nao wamemtaka Gavana Hassan Joho kukabiliana na tatizo la taka ili kukomesha mbu.

You can share this post!

RAMADHANI: Chunguza saum yako ukiwa katika ndoa ya aina hii

KURUNZI YA PWANI: Wautaja utalii ‘laana’ watoto wao...

adminleo