Makala

KURUNZI YA PWANI: Wautaja utalii ‘laana’ watoto wao wakigeuzwa makahaba

June 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

JAPO utalii unachangia pakubwa pato la uchumi wa taifa, umegueuka kuwa ‘laana’ kwa jamii zinazoishi Pwani baada ya baadhi ya watalii kugeuza wasichana wa shule kuwa makahaba na kuwadhulumu wengine kimapenzi.

Visa vya watalii kudhulumu watoto wa kati ya umri wa miaka 12 hadi 17 vimeongezeka katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale.

Katika hoteli za kifahari maandishi “Haturuhusu ngono za watoto” zimechapishwa kama njia moja ya kufanya kampeni ya kuangamiza dhuluma hii.

Lakini watalii hao wamevumbua njia mbadala, huwachukua watoto hao na kuwadhulumu kingono kwenye villa au vyumba maalum vya kukodi (apartment).

Mwezi wa Mei mwaka huu, mtalii raia wa Uingereza Keith Morris alipatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono watoto wa humu nchini.

Kesi ya mzee huyo mwenye umri wa miaka 72, ilisikizwa katika mahakama ya Uingereza baada ya upelelezi baina ya ofisi ya uchunguzi wa Uingereza ikishirikiana na ile ya humu nchini kupata ushahidi dhidi ya shutuma zilizokuwa zinamkabili.

Alipatikana na makosa tisa ya dhuluma za watoto huko Kilifi kwenye kesi.

Katika kijiji cha Maweni eneo la Kikambala kaunti ya Kilifi, mzungu huyo aliwalawiti watoto wengi.

“Alimlawiti mwanangu, tunashukuru haki imepatikana. Tulimjua kama mtu mzuri ambaye alikuwa anazuru eneo hili akifurahisha watoto wetu kumbe alikuwa na ila mbaya! Hatukumshuku,” akasema mzazi wa mtoto ambaye alilawitiwa na mzungu huyo.

Lakini mwaka jana, watu kutoka Nairobi walikuja kumhoji mwanangu.

Mtoto huyo alifichua kuwa mzungu huyo alikuwa anawapeleka matembezi eneo la Mombasa, baadaye kuwapeleka kuona sinema huko Nyali kisha anawapeleka katika chumba chake na kuwanajisi huko Bamburi.

Mtoto huyo alisema kila alipomkataza mzungu huyo dhidi ya uchafu huo alimsihi anyamaze wala asimwambie mtu yoyote.

Kisa hicho kilifanyika mwaka wa 2016.

“Kila siku alikuwa anatunajisi. Siwezi kukumbuka alininajisi mara ngapi. Alikuwa hatumii mpira. Ninashukuru haki imepatikana,” msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 akafichua.

Msichana huyo ni miongoni mwa mamia ya watoto waliopitia madhila miongoni mwa watalii wakongwe.

Lakini sasa bodi ya filamu nchini (KFCB) imeanza mikakati ya kukabiliana na dhuluma hiyo.

Meneja wa KFCB tawi la Pwani Boniventure Kioko alisema hulka hiyo inaendelea kushuhudiwa maeneo ya kitalii huku akiwataka wazazi kushirikiana katika kukomesha uchafu huo.

Kando na kudhulumiwa kingono, Bw Kioko alisema watoto hao hutumiwa kutengeneza filamu za ngono.

Naye afisa wa huduma za umma za vijana na jinsia (Public service, Youth and Gender Affairs CAS) Rachel Shebesh aliwataka kina mama kutunza watoto wao waendeleze masomo yao.