• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Mlima Kenya sasa wamlilia Raila

Mlima Kenya sasa wamlilia Raila

Na WAANDISHI WETU

WAZEE wa jamii ya Agikuyu Jumatatu walimlilia kiongozi wa ODM Raila Odinga wakimtaka amsaidie Rais Uhuru Kenyatta kukabiliana na ufisadi unaokumba asasi nyingi za Serikali.

Bw Odinga alikutana na viongozi hao wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Wakikuyu jana katika ofisi yake kwenye jumba la Capitol Hill, Nairobi.

Akijibu ombi lao, Bw Odinga aliwahakikishia kuwa anafanya kazi na Rais Kenyatta kwa karibu ili kuhakikisha wanaofuja mali ya umma wameadhibiwa kisheria.

“Ninawahakikishia kuwa ninaunga mkono kikamilifu vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi. Tulikubaliana na Rais Kenyatta kwamba wakati huu washukiwa hawatakuwa na mahali pa kujificha. Hawatajificha nyuma ya makabila yao au vyama vya kisiasa,” akasema Bw Odinga baada ya mkutano wa faragha na wazee hao.

Ahadi hiyo ya Raila ilijiri huku wabunge kadhaa wa chama cha Jubilee kutoka Rift Valley wakiendelea kulalamika kuwa juhudi zinazoendelea za kukabiliana na ufisadi ni njama inayolenga viongozi wakuu wa eneo hilo.

Viongozi hao walisema vita dhidi ya ufisadi vimegeuka kuwa uonevu wa kisiasa na kikabila unaolenga viongozi na maafisa wa serikali wa jamii chache, ili kuzima ndoto zao za kisiasa.

 

Ubaguzi katika vita dhidi ya ufisadi

Wabunge hao zaidi ya kumi waliapa kufichua stakabadhi zinazoonyesha viongozi wa jamii zingine pia waliohusika kwenye sakata kubwa za ufisadi ilhali hawaandamwi.

“Kile tunachoshuhudia ni ubaguzi katika utendaji wa haki katika vita dhidi ya ufisadi. Asasi zinazochunguza ufisadi zimefanya suala hili liwe la kulenga viongozi fulani wa jamii moja,” wakadai viongozi hao wakiongozwa na Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei.

Walilalamika kuhusu sakata ya ununuzi wa mahindi na kudai kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zilikuwa zikifuata wakulima na wafanyabiashara wadogo huku wahusika wakuu wakiachwa huru.

“Ingawa tunamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika kupambana na ufisadi, watu waliotajwa kwenye sakata hizo wanafaa waadhibiwe kisheria bila kujali makabila yao,” akasema Mbunge wa Tindiret, Bw Julius Melly.

Msimamo wao ulitangazwa huku EACC ikihoji watu wanne wenye ushawishi mkubwa katika jamii kwa kushukiwa kuhusika kwenye sakata ya uuzaji wa mahindi kwa njia za utapeli kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

 

Ni mapema

“Ni kweli kuna maafisa wetu wanaendeleza uchunguzi., lakini bado ni mapema mno kuanza kubahatisha kuhusu uzito wa upelelezi wetu,” Naibu Mkurugenzi wa EACC anayesimamia eneo hilo Jackson Mue alisema.

Afisa huyo alifichua kuwa wapelelezi walikusanya stakabadhi muhimu ambazo zinafanyiwa uchanganuzi.

“Tunataka kutambua kama wakulima halisi walinyimwa nafasi ya kuuzia NCPB mahindi na badala yake wafanyabiashara wakanufaika, na pia kama kulikuwa na ulaji rushwa katika shughuli hiyo,” akasema Bw Mue.

Lakini viongozi wengine wa eneo hilo walikashifu wanasiasa hao kwa kuingiza siasa na ukabila katika suala hilo.

“Hawa viongozi wanafaa kusema wazi ni akina nani hasa katika jamii zao wanaoshuku wanalengwa kwenye vita dhidi ya ufisadi badala ya kujaribu kuwatetea wandani wao,” akasema katibu wa ODM anayesimamia masuala ya ugatuzi, Bw Kipkorir Menjo.

Alipuuzilia mbali wito wa viongozi hao kuvunja EACC akasema vita dhidi ya ufisadi havihusu kabila wala vyama vya kisiasa.

Wazee hao walimpongeza Bw Odinga kwa kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta kwa lengo la kuunganisha Wakenya na kuleta amani nchini.

Baraza hilo pia lilipongeza baba yake Bw Odinga, Jaramogi Oginga Odinga kutokana na juhudi zake za kupigania uhuru na kushinikiza kuachiliwa kwa Mzee Jomo Kenyatta kutoka katika kizuizi cha wakoloni.

 

Ushirikiano kutokomeza zimwi 

“Tunakusihi utumie uhusiano wako mwema na Rais Kenyatta kukabiliana na ufisadi ambao umekithiri nchini na kuendeleza juhudi za kudumisha amani nchini,” akasema Bw Mwangi.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Wakikuyu walipongeza juhudi za Bw Odinga na Rais Kenyatta za kutaka kuunganisha Wakenya.

Sakata za ufisadi, katika siku za hivi karibuni, zimeripotiwa katika mashirika mbalimbali ya serikali, likiwemo Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ambapo Sh9 bilioni zinadaiwa kuibwa. Washukiwa 46 wamekamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya kuhusika na sakata hiyo.

Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB) imekumbwa na sakata ya wizi wa mabilioni ya fedha za wakulima wa mahindi.

Kitita cha Sh95 bilioni pia zinadaiwa kupotea katika Shirika la Kusafirisha Mafuta (KPC)

Wazee hao waliunga mkono vita dhidi ya ufisadi huku baadhi ya wandani wa Naibu wa Rais William Ruto wakidai kuwa operesheni ya kuwanasa wafisadi inayoendeshwa na serikali inalenga kutatiza azma ya kiongozi huyo kuingia ikulu 2022.

Wanasiasa hao, wengi wao kutoka Bonde la Ufa wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei, wikendi walidai kuwa vita dhidi ya ufisadi huenda vikasambaratisha ndoto ya Bw Ruto ya kumrithi Rais Kenyatta 2022 kwa kuwa vinaonekana kulenga maafisa wanaoegemea upande wa Naibu wa Rais.

Bw Ruto alipokuwa akizungumza katika eneobunge la Nyali, Kaunti ya Mombasa, Jumapili, alipuuzilia mbali madai hayo na akawataka wanasiasa hao kukoma kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

 

LEONARD ONYANGO, BARNABASI BII na TITUS OMINDE

You can share this post!

Flash ndiye bingwa wa mbio za magari 2018

Genge laiba ng’ombe 8 na kuwachinja kwa mochari

adminleo