Habari MsetoSiasa

Kalonzo na Moi wapanga kuungana wakilenga 2022

June 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BONIFACE MWANIKI

SENETA wa Baringo Gideon Moi na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, wameanza mikakati ya kutaka kubuni muungano mpya watakaotumia katika uchaguzi wa 2022.

Akizungumza katika mkutano wa kuchangisha fedha katika kanisa la AIC la Nuu, Mwingi ya Kati, ambapo alialikwa na seneta wa Kitui Enoch Wambua, mbunge wa Tiaty William Kamket, alisema Bw Musyoka na Gideon Moi wamelelewa kisiasa na Rais Mstaafu Daniel Arap Moi.

Alisema Rais Mstaafu anataka mwanawe Bw Gideon na Bw Kalonzo washirikiane katika uchaguzi wa 2022.

Bw Kamket alidai kuwa alipitia kwa Mzee Moi kabla ya kuelekea katika Kaunti ya Kitui ambapo alitumwa na Rais Mstaafu kwenda kumshawishi Bw Musyoka kuhusiana na uwezekano wa kutia saini mkataba wa maelewano wa kushirikiana katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kabla ya kuja hapa, nilimtembelea Mzee Moi nyumbani kwake Kabarak. Kwa kuwa mwana wenu Kalonzo Musyoka na Bw Gideon Moi ni watoto wake aliowakuza kisiasa, alinituma nimfikie Bw Musyoka na tuzungumze kuhusu kushirikiana katika kinyang’anyiro cha 2022,” akasema Bw Kamket.

Mbunge wa Tiaty alisema muafaka wa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga hauna uhusiano n uchaguzi wa 2022.

“Tuliona Rais Kenyatta akisalimiana na Bw Odinga jijini Nairobi, tunaunga mkono ushirikiano huo. Lakini muafaka huo hautuzuii kutafuta marafiki tutakaoungana nao kwa ajili ya uchaguzi ujao,” akasema.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema vyama vya Kanu na Wiper vimeanza mchakato wa kuunganisha viongozi wavyo ili kuhakikisha kuwa wanashinda uchaguzi wa 2022.

Bw Wambua alisema itakuwa vigumu kwa wawaniaji wengine kuwabwaga Bw Moi na Bw Musyoka ikiwa wawili hao wataungana.

“Bw Moi na Bw Musyoka wakiungana watafanikiwa kuingia Ikulu kwa urahisi katika uchaguzi wa 2022. Kadhalika, tunahitaji vigogo wengine wa muungano wa NASA, Bw Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula,” akasema Bw Wambua.

Alisema kushirikishwa kwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Bw Mudavadi na Wetang’ula w Ford-Kenya kutafanya muungano kuwa thabiti.

“Watu wangu, naomba ruhusa yenu niende kukutana na mzee Moi kwa niaba ya kiongozi wa chama chetu (Bw Musyoka) ili tuweze kuunda muungno utakaomwezesha kuingia ikulu baada ya uchaguzi ujao,” kasema Bw Wmbua.