Habari MsetoSiasa

Ruto aonya wanaovuruga muafaka wa Uhuru na Raila

June 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Mohamed Ahmed na Brian Ocharo

NAIBU Rais William Ruto, amewaonya wanasiasa ambao wanaendelea kuingiza siasa muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9 mwaka huu.

“Sharti tukomeshe siasa za chuki na siasa chafu ya vyama na tuunge umoja ambao unaongozwa na rais,” alisema Bw Ruto.

Bw Ruto alisisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi na viongozi wa Pwani kwa ajili ya maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo na kufikia azimio lake la mwaka wa 2022.

Hii ni baada ya baadhi ya viongozi wa kutoka eneo hilo kutangaza kuwa watashirikiana na Bw Ruto ili kuhakikisha anaingia mamlakani kama Rais katika mwaka wa 2022.

Jumatatu, wabunge wa eneo hilo pamoja na gavana wa Kwale Salim Mvurya walisema kuwa watahakikisha wanauza ajenda ya maendeleo ya Bw Ruto ili apate nafasi hiyo kwa urahisi ifikapo mwaka wa uchaguzi ujao ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo waliyoahidiwa na serikali ilioko mamlakani.

“Mimi nimekubaliana na viongozi wenu hapa kuwa tutafanya kazi pamoja. Sisi tutaleta maendeleo hapa na hatutosita mpaka tuone kila pembe imepata maendeleo hayo na mimi najua nyinyi wananchi muko na uhuru na muko na akili munajua ni nani wa kufanya kazi na yule waporojo na nyinyi munajua kuchagua na mutachagua,” akasema Bw Ruto.